NA ABOU KISANDU

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF) limeelezea sababu ya Zanzibar kutoshiriki Mashindano ya CECAFA Chalenji cup chini ya miaka 23 (U-23), yanayotarajiwa kufanyika Bahir Dar nchini Ethiopia kuanzia Julai 17, 2021 hadi Julai 31, 2021.

Meneja wa Leseni za klabu kutoka ZFF anaetambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) ambae pia ni Mwanasheria wa ZFF Mbarouk Othman Suleiman.

Alisema maradhi ya  Covid-19 ndio chanzo cha Zanzibar kujiondoa katika ushiriki wa mashindano hayo kutokana na uchumi kushuka.

“Unajua Corona imeathiri sana uchumi wa nchi mbali mbali ikiwemo  Zanzibar, kwa hiyo kifedha hatupo vizuri kwa sasa, kutokana na hali ya uchumi, tumeamua tusishiriki mashindano haya na sio sisi tu Zanzibar ambao hatushiriki, hata wenzetu Rwanda, Somalia na wengine wamejitoa”.alisema

Hadi juzi timu ya Taifa ya Zanzibar ilifanya mazoezi kujiandaa na mashindano hayo lakini baada ya Cecafa kupanga makundi, pamoja na kutoa ratiba ya mashindano hayo ambapo katika timu tisa zitakazoshiriki, Zanzibar haikuonekana ndipo kambi ya vijana wa Zanzibar ikavunjwa.

Cecafa imewapanga Kundi A Uganda, Tanzania bara na DR Congo ambapo kundi B wamepangwa wenyeji Ethiopia, Burundi na Eritrea huku kundi C

wakiwemo Djibouti, Sudan ya Kusini na Kenya.

Mashindano ya Cecafa Senior Chalenji cup mwaka huu hayotokuwepo ambayo ndio mashindano makubwa inayoshiriki timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes).

Badala yake Cecafa imeandaa mashindano hayo ya U-23 na ndio mashindano makubwa kwao kwa upande wa wanaume lakini Zanzibar haitoshiriki