NA MWANDISHI WETU

ALHAMDULILLAAH Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hajj ni aina mojawapo ya ‘ibaadah   bora kabisa na ni amali tukufu kabisa kwani ni mojawapo ya fardhi za Kiislamu ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemtuma Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutuongoza.  Dini ya mja wa Kiislamu haikamiliki bila ya Hajj.  Ni ‘ibaadah inayokubaliwa pindi yafuatayo yatahakikishwa:

Mtu ataifanyia bidii ya dhati kuwa ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee na kwa kutamani Aakhirah na haitowezekana kufanyika kwa ajili ya kumuonyesha mtu au kwa ajili ya maslahi ya dunia.

Inampasa mtu anapotenda ‘ibaadah yake afuate mfano wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa maneno na vitendo na hii haiwezekani kutimia ila kwa kujifunza na kupata elimu ya mafundisho ya Sunnah.

  Aina Za Hajj

Kuna aina tatu za Hajj; Tamattu’u, Ifraad na Qiraan.

Tamattu’

Hajji anavaa Ihraam ya ‘Umrah tu wakati wa miezi ya Hajj (anapokwenda Makkah mapema) ambayo inamaanisha kwamba anapofika Makkah atafanya twawwaaf na Sa’yi ya ‘Umrah. Kisha atanyoa au kukata nywele. Siku ya Tarwiyyah ambayo ni siku ya nane Dhul-Hijjah, atavaa nguo zake za Ihraam kwa ajili ya Hajj tu na atatekeleza yote yanayompasa kufanya.

Tamattu’

 Hajji anavaa Ihraam ya ‘Umrah tu wakati wa miezi ya Hajj (anapokwenda Makkah mapema) ambayo inamaanisha kwamba anapofika Makkah atafanya twawwaaf na Sa’yi ya ‘Umrah. Kisha atanyoa au kukata nywele. Siku ya Tarwiyyah ambayo ni siku ya nane Dhul-Hijjah, atavaa nguo zake za Ihraam kwa ajili ya Hajj tu na atatekeleza yote yanayompasa kufanya.

Ifraad:

Hajji atavaa Ihraam kwa ajili ya Hajj pekee.  Atakapofika Makkah atafanya twawwaaf pamoja na Sa’yi ya Hajj. Hana haja kunyoa au kukata nywele zake kwani hatoki kwenye Ihraam yake. Bali atabakia katika Ihraam mpaka amalize kurusha vijiwe katika Jamrah Al-‘Aqabah siku ya ‘Iyd. Anaruhusiwa kuchelewesha Sa’yi yake ya Hajj mpaka amalize twawwaaf ya Hajj.

QIRAAN:

Hajji anavaa Ihraam ya zote mbili; ‘Umrah na Hajj au anavaa kwanza Ihraam ya ‘Umrah, kisha anatia niyyah ya Hajj kabla ya twawwaaf ya Hajj. Wajibu wa anayefanya Ifraad ni sawa sawa na anayefanya Qiraan, isipokuwa tu mwenye kufanya Qiraan inampasa achinje na mwenye kufanya Ifraad haimpasi kuchinja

Aina ya Hajj iliyo bora kabisa katika hizi ni ya Tamattu’u ambayo ndio Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisisitiza ummah wake waitekeleze.

Hata kama Mweny kuhiji akitia niyyah ya kufanya Qiraan au Ifraad, anaruhusiwa kubadilisha niyyah yake kuingia katika Hajj ya Tamattu’u. Na anaweza kufanya hivi hata kama baada ya kufanya twawwaaf na Sa’yi kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofanya Twawwaaf na Sa’yi mwaka wa Hijjah ya Widaa’ (Hajj ya kuaga) pamoja na Maswahaba zake, aliamrisha wote ambao hawakuleta mnyama kwa ajili ya kuchinja, wabadilishe niyyah zao za Hajj na kutia niyyah ya ‘Umrah, wakate nywele zao, na wavue Ihraam mpaka Hajj.  Akasema:

“Ingelikuwa sikuleta mnyama ningelifanya hivyo nilivyokuamrisheni mfanye” [Al-Bukhaariy]  

‘UMRAH

Akipenda Hajji kuwa katika Twahaara ya ‘Umrah, akoge kama josho la janaba. Mwanamume atie manukato mazuri kabisa na apake mafuta mazuri kichwani. Hakuna ubaya harufu ikibakia baada ya Ihraam.

Kukoga ili kuingia katika Ihraam ni Sunnah kwa mwanamume na mwanamke pamoja na wanawake wenye hedhi na wale wenye Nifaas (damu ya uzazi).

Baada ya kukoga na kujitayarisha, Mahujjaaj wote isipokuwa wanawake wenye hedhi au nifaas wataswali Swalaah za fardhi inapowadia wakati wake kama kawaida. Na ikiwa sio wakati wa Swalaah ya fardhi basi ataswali Raka’h mbili ambazo ni vizuri mtu kuswali kila anapotia wudhuu.

Atakapomaliza kuswali atasema Talbiyah hii:

Labbayka-Allaahumma ‘Umrah, Labbayka-Allaahumma Labbayk. Labbayka laa shariyka Laka LabbaykInnal-Hamda Wan-Ni’imata Laka wal-Mulk laa shariyka Lak.

“Nimekuitikia Ee Allaah ‘Umrah, Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika, nimekuitika, hakika himdi na neema na ufalme ni Vyako Huna mshrika”

Mwanamume atasema kwa sauti na mwanamke atasema kiasi cha kumsikia wa pembezoni mwake. (Wanawake wenzake).

Anatakiwa mtu kusema Talbiyah kila mara khaswa anapofika na kubadilisha kituo. Mfano anapopanda na kushuka kipando wakati wa safari au wakati wa usiku unapoingia na asubuhi kunapopambazuka. Pia Amuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) radhi Zake za kupata Jannah na aombe kujikinga na moto kwa Rahmah Za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

Anatakiwa mtu aseme Talbiyah wakati wa ‘Umrah tokea anapovaa Ihraam yake hadi anapoanza Twawwaaf. Wakati wa Hajj aseme Talbiyah kutokea mwanzo wakati anapovaa Ihraam yake mpaka anapoanza kupiga mawe Jamarah ya ‘Aqabah siku ya ‘Iyd.

Hajji anapoingia msikitini atangulize mguu wake wa kulia na kusema:

A’uwdhu biLlaahil-‘Adhwiym, wabi Wajhihil-Kariym wa-Sultwaanihil-qadiym, minash-shaytwaanir-rajiym (BismiLLaah was-swalaatu) (was-salaamu ‘alaa Rasuwli-Llaah) Allaahummaftah-liy abwaaba Rahmatika

“Najikinga na Allaah Mtukufu, na kwa Wajihi Wake Mkarimu, na kwa utawala Wake wa kale, dhidi ya shaytwaan aliyeepushwa na Rahmah za Allaah (Kwa jina la Allaah na Swalaah na salaam zimfikie Rasuli wa Allaah) Ee Allaah nifungulie milango ya Rahmah Yako.”

Anakaribia Hajar Al-Aswad (jiwe jeusi) na kuligusa kwa mkono wake wa kulia na kulibusu. Ikiwa hii haiwezekani, basi aelekeze tu uso wake kuelekea kwenye Hajar Al-Aswad na kuashiria kwa mkono wake. (Usibusu mkono wako!) Haifai kusukuma na kusababisha madhara kwake na kwa watu.

Anapoligusa au kuliashiria Hajar Al-Aswad anatakiwa aseme hivi:

BismiLLaahi wa-Allaahu Akbar, Allaahumma Iymaanam-Bika, Wa taswdiyqam-bikitaabika, wa wafaa-aan bi’ahdiak, wat-tibaa’al-lisunnati Nabiyyika Muhammad Swalla Allaahu ‘Alayhi wasallam.

Kwa jina la Allaah, na Allaah ni Mkubwa, Ee Allaah kwa iymani Kwako, na kwa kuamini kitabu Chako, na kwa kutekeleza ahadi yako, na kufuata Sunnah ya Nabii Wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

(Tanbihi: Pamoja na Imaam kutaja ziada ya du’aa baada ya ‘BismiLLaahi Wa-Allaahu Akbar’(Kwa jina la Allaah, na Allaah ni Mkubwa), maelezo yaliyofuatia pamoja na kwamba yananasibishwa na Maswahaba ‘Aliy bin Abi Twaalib, Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar, lakini Wanachuoni wengi wa Hadiyth miongoni mwao Ibn Hajr na Al-Albaaniy wameeleza kuwa hazijathibiti kutoka kwao.)

Hajji lazima atembee huku Ka’bah liko kushotoni mwake. Anapofika Rukn Al-Yamani aiguse lakini asibusu bali atakapokuwa baina yake na Hajar Al-Aswad aseme:

(Rabbanaa Aatinaa fid-duniyaa Hasanatan wafil Aakiharati Hasanatan waqinaa ‘adhaaban-naar)).

“Rabb wetu, Tupe duniani mema, na Aakhirah mema, na Utulinde na adhabu ya moto”

Allaahumma Inniy As-alukal-‘afuw wal-‘aafiyata fid-duniyaa wal-Aakhirah

“Ee Allaah Nakuomba msamaha na al-‘aafiyah (afya, salama amani kutokana na kila shari na ovu) duniani na Aakhirah”

Kila mara akilipita Hajar Al-Aswad anatakiwa aseme “Allaahu Akbar”

Katika kufanya Twawwaaf zilizobakia anaweza kusema anachopenda katika Du’aa, kumtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kusoma Qur-aan.  Hii kwa sababu twawwaaf, Sa’yi na kurusha vijiwe Jamrah imekhusiwa kwa ajili ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

Katika Twawwaaf hii anahitajika mwanamume afanye vitu viwili:

Aweke Al-Idhwtwiba’a kutoka mwanzo wa Twawwaaf mpaka mwisho. Al-Idhwtwiba’a ina maana kwamba ni kuweka sehemu ya katikati ya vazi (ridaa) chini ya kwapa lake la kulia na kipande cha ridaa akipitishe juu ya bega la mkono wa kushoto. Anapomaliza kufanya Twawwaaf anaweza kurudisha ridaa yake katika hali yake ya mwanzo kwa sababu wakati wa Idhwtwiba’a ni wakati wa Twawwaaf tu.

Kufanya Ar-Raml katika Twawwaaf tatu za mwanzo. Ar-Raml ina maana kwamba kuzunguka kwa mwendo wa haraka kwa hatua ndogo ndogo. Kisha anatakiwa atembee mwendo wa kawaida katika Twawwaaf zake nne za mwisho.

Atakapomaliza mizunguko saba ya Twawwaaf, atakaribia Maqaam Ibraahiym na atasoma: fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni pahala pa kuswalia. [Al-Baqarah: 125]

Ataswali Raka’ah mbili fupi, akiwa karibu kiasi iwezekanavyo na nyuma ya Maqaam Ibraahiym. Katika Raka’ah ya mwanzo atasoma Swratul-Kaafiruwn na Raka’ah ya pili atasoma Suwratul-Ikhlaas. Atakapomaliza Raka’ah mbili atarudi kuligusa Hajar Al-Aswad kama itawezekana.   Atakwenda Al-Mas-‘aa, atakapofika karibu na As-Swafaa atasoma: Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah.  [Al-Baqarah: 158]

Atapanda (kilima cha) Swafaa mpaka aweze kuona Ka’abah. Aelekee Ka’abah na anyanyue mikono yake, amtukuze Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na aombe Du’aa apendayo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba:

Laa iIlaaha illa-Allaah Wahdahu laa shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Laa ilaaha illa-Allaah Wahdahu, Anjaza Wa’dahu Wanaswara ‘Abdahu Wahazamal-Ahzaaba Wahdahu.

 “Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, hali ya kuwa Peke Yake, wala Hana mshirika, Ufalme ni Wake na Himdi ni Zake, Naye juu ya kila kitu ni Muweza.  Hapana muabudiwa wa hakii ila Allaah hali ya kuwa Peke Yake, Ametekeleza ahadi Yake, na Amemnusuru mja Wake, na Amevishinda vikosi Peke Yake”

Atasema mara tatu akiomba Du’aa baina yake.

Atateremeka As-Swafaa na kuelekea Al-Marwah kwa mwendo wa kawaida mpaka anapofika katika alama ya kijani, hapo atatembea kwa mwendo wa kukimbia mpaka alama ya kijani nyingine.  Ataendelea kuelekea Al-Marwah kwa mwendo wa kawaida. Atakapofikia atapanda (kilima) na kuelekea Qiblah, atanyanyua mikono na kurudia kusema kama alivyosema alipokuwa As-Swafaa. Atateremka Al-Marwah kuelekea As-Swafaa, akihakikisha anatembea sehemu zinazohusika na kukimbia katika sehemu zinazohusika.

Ataendelea kufanya hivyo hivyo mpaka amalize mizunguko saba. Kutoka As-Swafaa kwenda Al-Marwah ni mzunguko mmoja na kurudi ni mzunguko mwingine. Wakati wa Sa’yi anaweza kusoma anachotaka kama Du’aa, Qur-aan na kumtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

Anapomaliza Sa’yi atanyoa nywele. Mwanamke atakata nywele kiasi cha urefu wa ncha ya kidole. Inapendekezeka kunyoa nywele zote, na kunyoa ni bora kuliko kukata kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaombea du’aa walionyoa mara tatu na waliokata mara moja. Isipokuwa ikiwa Hajj iko karibu na hakuna wakati wa kutosha kwa nywele kurudi kukua, basi ni bora kukata ili nywele zibakie kwa ajili ya kunyoa wakati wa Hajj, kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha Maswahaba kukata nywele katika ‘Umrah kwani walifanya asubuhi ya tarehe nne ya Dhul-Hijjah.

Baada ya hapo ‘Umrah itakuwa imemalizika na Hajji atakuwa huru kuvaa nguo nyingine, kutia manukato (mwanamume) na kurudia hali ya ndoa (kujimai na mkewe) na kadhalika.

 Siku Ya Tarwiyyah, Tarehe 8 Dhul-Hijjah 

Siku ya tarehe 8 Dhul-Hijjah, Hajji atajitoharisha tena kwa kukoga kama alivyofanya kabla ya ‘Umrah mahali hapo anapokaa.  Atavaa Ihraam yake na kusema:

Labbayka Hajja Labbayka-Allaahumma Labbayk, Labbayka, laa shariyka Laka Labbayk, innal-Hamdawan-Ni’mata Laka wal-Mulk, laa shariyka Lak

“Nimekuitikia Ee Allaah Hajj, Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika, nimekuitika, hakika Himdi na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshirika ”

Ikiwa atakhofu kuwa jambo litamzuia kukamilisha Hajj yake basi atie niyyah kwa kusema:

“Ikiwa nitazuiliwa na kizuizi chochote sehemu yangu ni popote nilipozuiliwa”

Ikiwa hana khofu kama hiyo basi hana haja kujishurutisha hivyo.

Kisha Hajji atakwenda Mina na huko ataswali Swalaah ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, ‘Ishaa na Al-Fajiri na kufupisha Swalaah za Raka’h nne kuwa mbili mbili kila moja bila ya kuziunganisha. (Yaani kuswali kila moja vile kwa wakati wake ila ziwe fupi tu) kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali Qaswran (kufupisha) na sio Jam’an (kujumuisha).

Tarehe 9 Dhul-Hijjah – Siku ya ‘Arafah

Jua litakapochomoza siku ya pili ambayo ni tarehe 9 Dhul-Hijjah, atakwenda ‘Arafah na huko ataswali Adhuhuri na Alasiri kwa kuunganisha wakati wa Adhuhuri na kufupisha mbili mbili. Atabakia katika msikiti wa Namirah mpaka jua litakapokuchwa. Atamdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  hapo ‘Arafah na kuomba Du’aa nyingi sana awezavyo huku akielekea Qiblah na sio kuelekea Mlima wa ‘Arafah.

Ikiwa atakuwa hakujaaliwa kuweko katika Msikiti wa Namirah karibu na Jabali la ‘Arafah basi popote alipokuweko kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama katika jabali la ‘Arafah na akasema:

((Nimesimama hapa na ‘Arafah yote ni kisimamo (cha ‘Arafah) na msisimame katika bonde la ‘Uranah))

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba:

 Laa ilaaha iIlla-Allaah Wahdahu laa shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr

“Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah hali ya kuwa Peke Yake, Hana mshirika, ni Wake Ufalme na ni Zake Himdi, Naye juu ya kila kitu ni Muweza”

Atakapochoka anaruhusiwa kuzungumza na wenzake au kusoma vitabu vyenye faida khaswa vile kuhusu ukarimu, utukufu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na neema kubwa za Allaah kwetu ili apate kuzidi kupata matumaini kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kisha arudi kuendelea kuomba Du’aa na kuhakikisha kuwa anatumia wakati wake wa mwisho wa siku hiyo katika Du’aa nyingi na nzito kwa sababu Du’aa zilizo bora kabisa ni Du’aa za siku ya ‘Arafah.

 Muzdalifah:

Jua litakapozama ataondoka ‘Arafah kwenda Muzdalifah na huko ataswali Magharibi, ‘Ishaa na Al-Fajiri Ikiwa atachoka au ana uchache wa maji, anaruhusiwa kuunganisha Magharibi na ‘Ishaa.  Ikiwa atakhofu kuwa hatofika Muzdalifah mpaka baada ya usiku wa manane, basi aswali kabla ya kufika huko kwani hairuhusiwi kuchelewesha Swalaah mpaka usiku wa manane.

Atabakia huko Muzdalifah akiomba Du’aa na kumtaja Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mpaka Alfajiri, ataswali Alfajiri mapema kwa adhaan na Iqaamah, kisha ataelekea Mash’aril-Haraam (sehemu tukufu) na atafanya tahliyl, yaani atasema “Laa ilaaha illa Allaah” pia “Allaahu Akbar”na ataomba Du’aa mpaka kupambazuke vizuri. Ikiwa hakujaaliwa kwenda Mash’aril-Haraam, ataomba hapo hapo alipo kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Na atakuwa akiomba Du’aa kwa kuelekea Qiblah na huku akinyanyua mikono.

Minaa – Ar-Ramiy (Krusha vijiwe) Katika Jamrah

Ikiwa ni mtu dhaifu na hawezi kustahamili  zahma za watu wakati wa Ar-Ramiy (kurusha vijiwe), (kama mwanamke na mtu mzima), basi anaruhusiwa kwenda Minaa mwisho wa usiku huo kupiga Jamrah kabla ya zahma ya watu kuwa kubwa.

Tarehe 10 Dhul-Hijjah:

Karibu na jua kuchomoza Hujaji ataondoka Muzdalifah kuelekea Minaa. Atakapofika atafanya yafuatayo:

Atarusha vijiwe saba moja moja katika Jamrah ya ‘Aqabah ambayo iko karibu na mnara wa Makkah na kusema :

Allaahu Akbar

Kwa kila kijiwe anachokirusha.

Atachinja mnyama, na kula baadhi ya nyama na atatoa nyingine kuwapa masikini. Kuchinja ni fardhi kwa wale wanaofanya Hajj ya Tamattu’u na Qiraan. (Kwa hali ilivyo sasa huwa haiwezekani kufanya hivi, hivyo anaweza kutekeleza kama anavyoamrishwa yaani kulipa na kuacha jukumu hili kwa serikali ifanye kazi ya kuchinja)

Mambo matatu hayo yafanywe kama ilivyo taratibu yake ikiwezekana, lakini hakuna kikwazo au sharti ikiwa mtu atatanguliza kitendo chochote kabla ya chengine.

Akimaliza hayo mambo matatu anaruhusiwa kujitoa katika Ihraam. Na anaweza kuvaa nguo zake za kawaida na kufanya kila jambo la halaal ila kuingia katika kitendo cha ndoa.

Atakwenda Makkah kufanya Twawwaaful-Ifaadhwah na Sa’yi kwa ajili ya Hajj. Ni Sunnah kujitia manukato kabla ya kwenda Makkah (kwa wanaume) kutokana na kauli ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba:

((Nilikuwa nikimpaka manukato Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kuingia katika Ihraam na na baada ya kutoka katika Ihraam kabla ya kutufu Ka’aba)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Atakapomaliza Twawwaaf na Sa’yi, Hujaji anaruhusiwa kufanya kila kitu kilicho halali hata tendo la ndoa.

Tarehe 11 na 12 Dhul-Hijjah:

Baada ya kufanya Twawwaaf na Sa’yi atarudi Minaa kulala huko usiku wa tarehe kumi na moja na wa kumi na mbili Dhul-Hijjah.

Atarusha vijiwe Jamrah tatu jioni zote za siku ya tarehe kumi na moja na kumi na mbili Dhul-Hijjah. Ataanza kwanza Jamrah ya kwanza ambayo iko mbali na Makkah, kisha ya katikati, kisha ya mwisho Jamrah Al-Aqabah.

Katika kila moja ya Jamrah atarusha vijiwe saba moja moja na huku atasema Takbiyr kwa kila kijiwe anachokirusha.

Atasimama baada ya kurusha vijiwe Jamrah ya kwanza na ya katikati kufanya Du’aa akielekea Qiblah akiwa amenyanyua mikono na kuomba Du’aa ndefu akiweza kufanya hivyo, au asimame kadiri atakavyoweza. Wala haimpasi kuacha kuomba Du’aa kwani ni Sunnah na watu wengi sana hawatekelezi hivi aidha kwa kutokujua au kupuuza. Na kila inapokuwa Sunnah haitekelezwi huwa kutangazika kwake kwa watu na kutendeka huenda ikaachwa kabisa na kupotea.

Hairuhusiwi kurusha vijiwe kabla ya Adhuhuri katika siku mbili hizi. 

Ni bora kabisa kutembea kwenda kurusha vijiwe, ingawa kipando kinaruhusiwa. 

Ikiwa mtu ana haraka baada ya kurusha vijiwe siku ya kumi na mbili Dhul-Hijjah, anaweza kuondoka Minaa lakini iwe kabla ya jua kuzama. Lakini akipenda kuzidisha makazi yake, ambayo ni bora zaidi, basi alale Minaa usiku wa kumi na tatu na arushe mawe jioni kama alivyofanya siku ya kumi na mbili.

Twawaaful-Widaa’ (Twaaf Ya Kuaga):

Atakapokuwa tayari kurudi kwao, atafanya twawwaaful-Widaa’ ambayo ni mizunguko saba katika Ka’abah kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Asikimbie mtu (asiondoke zake) mpaka iwe shughuli yake (kitendo chake cha mwisho) katika Nyumba (Ka’abah)) [Muslim]

Wanawake wenye hedhi na nifaas hawana lazima kufanya Twawwaaful-Widaa’i kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

((Aliamrisha watu iwe shughuli zao za mwisho ni Ka’abah isipokuwa waliruhusiwa (wanawake) wenye hedhi)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ikiwa baada ya twawwaaful-Widaa’i umebakia wakati wa kusubiri wenzake au kipando chake au kununua kitu njiani hakuna neno juu yake, wala hana haja ya kurudia kufanya Twawwaaful-Widaa’i isipokuwa akitia niyyah ya kuchelewesha safari yake, mfano akitaka kuondoka mwanzo wa siku akatufu Ka’abah, kisha akachelewesha safari yake hadi mwisho wa siku, basi itamlazimu arudie kufanya Twawwaaf ili kiwe kitendo chake cha mwisho ni Ka’abah.