HARARE, ZIMBABWE

RAIS wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema kwamba serikali yake inalenga kutoa chanjo za covid 19 kwa watu milioni moja katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Kiongozi huyo pia aliongeza muda wa kufungwa kwa shughuli za kawaida kwa siku 14 zaidi. Kutokana na ongezeko jipya la maambukizi ya virusi corona pamoja na vifo nchini humo.

Mnamo Juni 29 mwaka huu rais Mnangagwa aliweka kanuni mpya kali zikiwemo amri ya kutotoka nje nyakati za usiku pamoja na kuzuia usafiri kati ya miji ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Mnangagwa alisema kuwa maambukizi ya corona yanaongozeka kwa kasi kutokana na aina mpya ya virusi vya delta.

Alisema wanalenga kutoa chanjo kwa watu milioni moja kabla ya kufunguliwa tena kwa shughuli za kawaida.

Kufikia sasa, taifa hilo liliopo kusini mwa Afrika limeshuhudia maambukizi zaidi ya watu 70,000, robo yake yakiwa yametokea katika muda wa wiki mbili zilizopita.

Vifo 2,236 pia vimeshuhudiwa katika muda huo. Tangu zoezi la utoaji chanjo za covid lilipoanza nchini humo, ni watu takriban 900,000 waliopata kufikia sasa.

Wiki iliyopita, Mnangagwa kupitia hotuba kwa njia ya televisheni alisema kuwa ripoti iliyotolewa wiki iliyopita inasema kuwa asilimia 80 ya maambukizi mapya ya corona ni kutokana na virusi vipya vya delta.

Katika kipindi cha wiki moja taifa hilo lilipata dozi milioni mbili za covid wakati nyingine milioni 3.5 zikitarajiwa kuwasili nchini humo mwishoni mwa mwezi huu.