HARARE, ZIMBABWE

KUNDI moja la mazingira nchini Zimbabwe limeishitaki serikali kutokana na mpango wake wa kupeleka ndovu nchini China.

Huku kundi hilo la Advocates4Earth, likiilaumu China kwa kuweka ndovu kwenye mazingira hatari ya kiafya.

Katika hati ya mashitaka iliowasilishwa mbele ya mahakama kuu, Advocates4Earth linaomba mamlaka ya kitaifa ya wanyama pori ya Zimbabwe izuiliwe kupeleka ndovu nchini China.

Lenin Tinashe Chisaira ambaye ni kiongozi wa Advocates4Earth amesema kuwa wanacholenga ni kuomba mahakama itoe amri kwamba serikali ya Zimbabwe na wakala wake waheshimu sheria za kimataifa kwamba ndovu wa Afrika au wanyama wengine, wasipelekwe kwenye mataifa ambayo hayana mazingira asilia kwao.

Amesema kwamba wanahisi kuna baadhi ya idara za serikali zinakusudia kukiuka kanuni hizo kwa kupeleka wanyama pori kwenye mataifa kama China bila kuzingatia mikakati ya kisheria.

Huku ikielezwa kuwa mashitaka ya Advocated4Earth pia yanamjumuisha waziri wa mazingira ,Nqobizitha Mangalisi Ndlovu.

Aidha idadi ya ndovu nchini Zimbabwe imeongezeka maradufu katika miaka ya karibuni na kufikia takriban laki moja, suala ambalo limesababisha baadhi ya wakulima kulalamika kuwa wanaharibu mimea pamoja na malisho ya mifugo yao.

Licha ya mashitaka yaliowasilishwa , idara ya kitaifa ya wanyamapori ya Zimbabwe imekanusha kwamba inapanga kupeleka ndovu China.

Tinashe Farawo ambaye ni msemaji wa idara hiyo amesema kuwa hao ni watu wanaotafuta umaarufu, akiongeza kuwa kwenye hotuba ya Rais Emmerson Mnangagwa kwa taifa, alitoa onyo kwa watu wa aina hiyo.

Katika kipindi cha nyuma, Zimbabwe imepeleka ndovu kwenye mataifa mengine licha ya kuwepo malalamiko kutoka kwa wanaharakati wa haki za wanyama kama vile Advocates4Earth.