Ndani ya dakika 15 kutoa vibali kwa wawekezaji
NA ABOUD MAHMOUD
USHIRIKIANO baina ya Taasisi ya Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuzaji Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) yatasaida kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk Muhudu I Kazi wakati alipofika katika ofisi za ZIPA na ujumbe aliofuatana nao zilizopo Maruhubi nje kidogo ya mji wa Unguja kwa ajili ya kukutana na viongozi wa ofisi hiyo ili kuendeleza ushirikiano.
Dk. Muhudu alisema bado kuna maendeleo ambayo yanahitaji kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kupatikana kwa mafanikio ambayo yatasaidia kuitangaza Tanzania kitaifa na kimataifa.
Alisema ujio wao huo utasaidia katika kujifunza mambo mbali mbali ambayo yanafanywa na ZIPA na yameweza kuondosha changamoto mbali mbali kwa wawekezaji.
“Ziara yetu hii imelenga kuja kujifunza pamoja na kuendeleza mashirikiano baina ya TIC na ZIPA ambayo yatasaidia kuinua uchumi wa nchi yetu pamoja na kupatikana mafanikio tulioyakusudia,”alisema.
Aidha, Dk .Muhudu, aliwaomba wafanyakazi wa ZIPA kuzidisha mashirikiano pamoja na kuwapa taaluma TIC ambayo itasaidia kwenda na wakati katika kutoa huduma kwa wawekezaji nchini.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Shariff Ali Shariff, alisema anamini mashirikiano kati ya taasisi hizo mbili ni kupatikana kwa manufaa ambayo yataweza kusaidia kuinua uchumi wa taifa.
Shariff alisema kwa muda mrefu Zanzibar ilikua ikitegemea utalii, lakini kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa corona nchi nyingi ziliathirika ikiwemo Zanzibar kutokana na watalii wengi kushindwa kusafiri.
Aidha, hivi sasa alisema suala la uchumi wa buluu limepewa kipaombele na hivi wanajiandaa kutangaza maeneo ambayo yatasaidia kuvutia watalii katika bahari.