Wananchi shehia husika watakiwa kutoa ushirikiano
Lengo ni kutokomeza kipindupindu Zanzibar
NA MOHAMMED SHARKSY (SUZA)
ZOEZI la chanjo ya kipindupindu hapa Zanzibar linaanza leo katika baadhi ya maeneo ya Unguja na Pemba.
Utoaji huo wa chanjo ni moja ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ambao umekuwa ukiisumbua sana Zanzibar kwa miongo kadhaa.
Karibu kila msimu wa mvua hasa zilizoongoka hapa Zanzibar wagonjwa wa kipindupindu huripotiwa lakini kwa muda sasa hakuna kesi za ugonjwa huo.
Ili kuona ‘Bila ya kipindupindu Zanzibar inawezekana’ kwa makusudi serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO) limeamua kudhibiti ugonjwa huo.
Zoezi hilo la chanjo litaendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza linatarajiwa kuanzia leo Julai 3 ikiwahusisha wananchi zaidi ya 327,000 wanaosihi katika shehia hatarishi za uwepo wa ugonjwa huo.
MAENEO YATAKAYOTOLEWA CHANJO
Maeneo hayo ni pamoja na Wilaya ya mjini ambapo mitaa kama ya Shauri moyo, Muembe makumbi, Chumbuni, Kwamtipura, Amani, Kilmahewa bondeni na Jan’gombe, huku Wilaya ya magharibi “B’’ Shehia ya Kinuni, Dimani, Mwanakwerekwe, Magogoni, Fuoni kibondeni, Tomondo na Meli nne watu watapewa chanjo hiyo.
Aidha maeneo mengine ni wilaya ya Magharibi “A” ambapo maeneo ya Mtopepo, Mwera, Mtoni, Bububu, Welezo na Mtoni kidatu, huku Wilaya ya Kaskazini “A” itahusisha Shehia ya Mkokotono, Kikobwweni na Banda maji, ambapo Wilaya ya Kaskazini “B” Shehia ya Mangapwani watu wake watapatiwa chanjo hiyo.
Pia Wilaya ya Kusini katika Shehia ya Kitogani na Muungoni, huku Wilaya ya Kati ikihusisha Shehia ya Ukongoroni.
Aidha zoezi hilo pia litatolewa katika kisiwa cha Pemba ambapo Wilaya ya Micheweni Shehia ya Kiuyu Mbuyuni, Maziwa n’gombe na Micheweni na Wilaya ya Wilaya ya Wete Shehia ya Kojani, Mpambani na Kiuyu Minungwini.
Katika kulitekeleza zoezi hilo tunawanasihi wananchi walengwa wa maeneo tengefu ya chanjo kutoa ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na kukubali kupokea
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII ZANZIBAR

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alisema serikali kupitia wizara yake inakusudia kutoa chanjo ya kipindupindu ambayo ni salama na wala haina tatizo lolote.
Alisema zoezi hilo la chanjo litaendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza linatarajiwa kufanyika Julai 3 na 7 mwaka huu ikiwahusisha wananchi zaidi ya 327,000 wanaosihi katika shehia hatarishi za uwepo wa ugonjwa huo.
Aidha Mazrui alisema wizara yake na serikali ya Mapinduzi kwa ujumla itaendelea kushirikiana na shirika la WHO katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wananchi.
Alisema katika mkakati wa serikali ya kuondosha ugonjwa wa kipindupindu Zanzibar, WHO imeona ipo haja ya kuisaidia Zanzibar kwa kuipatia misaada mbalimbali ikiwa na lengo la kuhakikisha ugonjwa huo unakuwa historia.
“Shirika la WHO limekuwa na jitihada mbalimbali katika kuisaidia Zanzibar katika kuhakikisha matatizo mbalimbali ya kiafya kwa wananchi yanaondoka”, alisema.
Aidha alisema, kupatiwa chanjo hiyo kutasaidia Zanzibar kupungua kwa maradhi ya mripuko ya kipindupindu katika shehia zinazosifika kwa ugonjwa huo ambapo alisema kukabidhiwa vifaa hiyo kutasaidia kutangaza vyema jinsi ya kujikinga na miripuko.
Hivyo, aliliomba shirika hilo, kuendelea kuisadia Zanzibar kwani wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ambapo wananchi wamekuwa wakifaidia na shirika hilo.
Sambamba na hayo, aliwataka wananchi kwenye shehia zitakazohusika na zoezi hilo kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha malengo ya serikali kutokomeza kipindupindu hapa Zanzibar.
SHIRIKA LA AFYA DUNIANI (WHO) ZANIZBAR
Mwakilishi mkaazi wa Shirika la Afya duniani Ofisi ya Zanzibar, (WHO), Dk. Andemichael Ghirmy, alisema shirika hilo litaendelea kutoa msaada mbalimbali kwa wananchi wa Zanzibar.
Aidha alimuhakikishia Waziri wa Afya, kuendelea kushirikiana na serikali ya Zanzibar katika kusaidia juhudi za kukinga maradhi mbalimbali licha ya kuwa Zanzibar haipo katika hali mbaya.
Alisema chanjo hiyo imeshafanyiwa utafiti wa kutosha na kuidhinishwa na shirika hilo ambapo kwa sasa nchi kadhaa zinazosumbuliwa na ugonjwa huo zimeshatolewa na hakuna tatizo la aiana yoyote.
Sambamba na hilo, alisema kuwa Chanjo hii imeshawahi kutolewa katika nchi mbalimbali kama vile Ethiopia, Zambia, Msumbiji nakadhalika ambapo hadi sasa nchi hizo hazijaripoti matatizo yoyoye yanayohusiana na chanjo hizo.
Hatua hiyo imeipelekea Shirika la Afya Duniani (WHO), kuuweka ugonjwa huu kama mojawapo ya viashiria vya maendeleo ya jamii husika.
WITO KWA WANANCHI KUHUSIANA NA CHANJO YA KIPINDUPINDU
Katika kulitekeleza zoezi hilo, serikali inawanasihi wananchi walengwa wa maeneo tengefu ya chanjo kutoa ushirikiano wa dhati ikiwa ni pamoja na kukubali kupokea chanjo hiyo jambo ambalo litawaondoshea adha ya mara kwa mara kuugua kipindupindu.
Wananchi hawapaswi kuogopa kwa kuwa Chanjo hiyo ni ya kunywa na ina dozi mbili ambapo dozi ya kwanza inaanza leo huku dozi ya pili ikitolewa 31/7-4/8/2021.
Kwa mujibu wa wataalamu Chanjo ya kwanza hutoa kinga ya miezi 6 na unapokamilisha chanjo ya Pili basi utapata kinga ya miaka 3.
Chanjo hii ya kipindupindu inahusisha watu wote waliofikisha umri wa mwaka 1 na kuendelea pamoja na Wazee na wenye magonjwa ya muda mrefu au kwa jina jengine magojwa sugu pia wanaweza kupata chanjo hii.
Watu ambao hawatalazimika kupewa chanjo hiyo ni watoto chini ya umri wa mwaka mmoja na akinamama wajawazito.
HISTORIA YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU ZANZIBAR
Zanzibar ni moja kati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zinakumbwa na magonjwa ya miripuko ya mara kwa mara na kupoteza wananchi wake ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Miripuko hii pia huathiri miundombinu ya kiuchumi ambapo kipindupindu ni kati yaugonjwa sugu na kuathiri jamii na maisha yao kwa ujumla.
Historia inatuonesha kwamba Zanzibar ilianza kukumbwa na maradhi Kipindupindu tokea kipindi cha miaka ya ukoloni, yaani 1800. Tokea kipindi hicho jumla ya miripuko 19 mikubwa ya ugonjwa huu imeripotiwa na zaidi ya wagonjwa 14,364 na kati ya hao 489 walipoteza maisha hii ni sawa na asilimia 3.6
Aidha inasemekana kwamba mripuko wa kwanza ulitokea katika robo ya mwisho ya karne 19, baadhi ya waandishi walieleza kwamba mripuko huo ulitokea katika mwaka 1888.
Katika mripuko huu ilikisiwa kwamba watu wengi (kwa maelfu), walifariki na walizikwa katika maeneo mbali mbali katika sehemu karibu na fukwe za bahari na katika maeneo ya Ng’ambo.
Mripuko mdogo ulitokea katika kisiwa cha Tumbatu mwanzoni mwa mwaka 1978 ambao uliwasibu wavuvi waliokwenda kuweka dago katika maeneo ya pwani ya Dar es Salaam.
Mripuko wa pili mkubwa ulitokea Mjini Unguja hapo Machi, 1978, ambapo watu wengi waliathirika na ugonjwa ulienea hadi katika baadhi ya mashamba yaliyo karibu na Mjini.
Imeelezwa kuwa sehemu zilizoathirika sana ni Saateni kwa barabara ya Kaskazini, Amani, Viwanda Vidogo Vidogo kwa njia ya kuelekea upande wa mashariki, Magomeni “Round About” barabara inayoelekea Kusini na Kiembesamaki barabara inayoelekea Fumba.
Inakisiwa kuwa zaidi ya watu 411 waliuguwa katika kipindi hicho na watu 51 walifariki dunia baada ya kukumbwa na maradhi hayo.
Aidha, mripuko huo mkuu wa mwaka 1978, mripuko mwengine mkubwa wa kipindupindu ulitokea mwaka 1998 na baada ya hapo miripuko ikitokezea takriban kila mwaka na ilisababisha vifo na athari mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Hivyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, mwishoni mwa mwaka 2018 ilizindua rasmi mpango shirikisha wa kitaifa wa kutokomeza kipindupindu hapa Zanzibar -ZACCEP.
HISTORIA YA KIPINDUPINDU DUNIANI
Historia ya kuwepo kwa maradhi ya Kipindupindu ni ndefu ambapo baadhi ya wataalamu wanaeleza kwamba maradhi hayo yalianza kujitokeza na kutambulikana tangu mwaka 1000 AD, sawa na kusema miaka 1,019 iliyopita.
Baada ya hapo maradhi hayo yaliripotiwa kujitokeza katika nchi mbali mbali duniani kwa miongo tafauti ambapo hata hivyo baada ya hapo maradhi hayo yaliripotiwa kujitokeza katika nchi mbali mbali duniani kwa miongo tofauti.
Hata hivyo, umaarufu wa maradhi haya ulienea pale ambapo ukubwa wa athari zake kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani ulianza kujulikana. Huu ulikuwa wakati ambao miripuko mikubwa ya kipindupindu iliibuka katika eneo la Bengal nchini India (Ganges Delta), karibu na mji wa Calcutta (Kalkata), kuanzia mwaka 1817 hadi 1824.
Katika kipindi hicho, maradhi hayo yalisambaa na kuathiri nchi mbali mbali duniani. Kwa hivyo, baadhi ya wataalamu wanahusisha mripuko huo mkubwa na historia ya kujulikana kwa maradhi haya.
Tangu mwaka 1817 hadi mwaka 1975 jumla ya miripuko saba mikubwa iliyoenea katika mataifa mbali mbali kwa kipinidi kimoja imeshatokezea. Miripuko hio imesababisha athari kubwa za kiuchumi na kijamii pamoja na kuteketeza idadi kubwa ya watu duniani.
VIPI MAAMBUKIZI YA KIPINDUPINDU HUPATIKANA
Ugonjwa huu hutokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binaadamu uletwao na vimelea vya bacteria vijulikanavyo kitaalamu kama Vibrio Cholerae.
Kwa kawaida vimelea hawa hupendelea kuishi katika kinyesi cha binaadamu ambapo mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea hivi vya kipindupindu.
Mara baada ya kula chakula au kunywa maji yaliyochafuliwa, baadhi ya vimelea huuwawa kwa tindikali iliyokwenye tumbo pindi chakula au maji haya yanapoingia tumboni lakini hata hivyo baadhi ya vimelea hawa hufanikiwa kukwepa ukali wa tindikali hii na hivyo kuendelea kuishi.
Vimelea waliofanikiwa kuepuka tindikali ya tumbo la binaadamu, hujongea kwenda kwenye ukuta wa utumbo mdogo kwa kutumia maumbo maalum yaliyo kwenye miili ambayo huwawezesha kusafiri ama kwa kitaamu huitwa flagella.
Wawapo kwenye ukuta wa utumbo mdogo Vibrio Cholerae hutoa sumu iitwayo CTX au CT (Cholera Toxin), ambayo husababisha mtu kuharisha choo chenye majimaji, papo hapo huendelea kutoa kizazi kingine cha vimelea hao nje kwa njia ya haja kubwa.
Iwapo choo hicho cha mtu aliyeambukizwa kipindupindu kitachanganyika na chanzo cha maji au chakula, watu wengine huambukizwa kirahisi.
Hali kadhalika iwapo kwenye choo ambacho hakipo kwenye mazingira ya usafi kuna hatari ya choo cha mwambukizwa kuchangayika na chanzo cha maji au chakula na hivyo kupelekea watu wengi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu.
NINI KIFANYIKE KUTOKOMEZA KIPINDUPINDU ZANZIBAR
Kwa kuwa Serikali ikishirikiana na wadau wa kimaendeleo kama WHO inajitahidi kuchukua juhudi za kupamabana na kipindupindu ikiwa ni hii ya kutoa chanjo basi shehia husika hazinabudi kutoa ushirikianao.
Aidha Serikali ichukuwe hatua ya kuimarisha miundombinu na kuhakikisha usafi wa mazingira unaendelezwa, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo baadhi ya wananchi hawazingatii matumizi mazuri ya miundombinu hio.
Ni muhimu tukafahamu kwamba kuna mambo mengine ambayo wananchi wenyewe wanapaswa wayafanye majumbani mwao, ili kuzilinda afya zao na familia zao, lakini kwa bahati mbaya wananchi hao hawafanyi hivyo.
Hata vyoo baadhi yao hawachimbi na karo za kupokelea maji machafu jambo ambalo linauwezekano mkubwa wa kusababisha ugonjwa wa kipindupindu.
Kadhalika, baadhi ya wafanyabiashara hasa wa vyakula, huendesha biashara zao bila ya kuzingatia mambo ya msingi ya usafi wa mwanadamu na mazingira yanayomzunguka, ambayo ni kwa maslahi yetu wenyewe.
Hivi sasa, baadhi ya wafanyabishara wamekuwa ni watu wa kulazimishwa kuangalia usafi. Kila siku wanasubiri wazozane na wakati mwengine wagombane na wafanyakazi wa Mabaraza ya Miji na Halmashauri, ndipo wazingatie taratibu za msingi za usafi.
Wafanyabiashara hao wanashindwa hata kuyasafisha maeneo na vifaa wanavyoendeshea shughuli zao. Hawataki kufahamu kwamba suala la kutunza usafi ni muhimu kwa ukuaji wa biashara wanazoendesha na afya za wananchi kwa jumla.
Ili kuona Zanzibar bila kipindupindu inawezekana’ wananchi wa maeneo husika ya chanjo hawanabudi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa zoezi hilo linaloanza leo.