NA MADINA ISSA
IDARA ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, imetoa mafunzo ya lugha ya alama wafanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa lengo la kuwasaidia kutoa huduma kwa jamii ya watu yenye ulemavu wa uziwi kuendelea kupata huduma stahiki wanapofika katika taasisi za serikali na binafsi.
Akifunga mafunzo hayo, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Khadija Rajab Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Madawa ya Kulevya, Haji Hamza Khamis, alisema lengo la serikali ni kuona wananchi wake wanapatia huduma zilizo bora katika taasisi mbalimbali bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Aidha alifahamisha kuwa lugha ya alama ni nyenzo ya kurahisisha mawasiliano baina ya wahitaji kwani imekuwa na umuhimu katika jamii, hivyo, ni vyema kujifunza ili kuisaidia jamii ya watu wenye ulemavu wa uziwi katika kutoa huduma mbali mbali.
Alisema ni jambo la kupongezwa kwa mfuko huo kuona umuhimu wa kuwasomesha wafanyakazi wake ambapo ni miongoni mwa taasisi zinazotoa huduma kwa jamii, ili ziwe imara zaidi.
“Ikiwa mtu mwenye ulemavu wa uziwi akifika ZSSF imani yetu ataweza kuhudumiwa kwa umakini kwani wafanyakazi wameiva kwa awamu ya kwanza na wakijiendeleza wataweza kutoa huduma stahiki” alisema.
Nae, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Mfuko huo, Dk. Hudda Ahmed Yussuf, alisema kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo, aliahidi kwa wafanyakazi wa taasisi yake, kuona huduma wanazozitoa zinakuwa za kiwango kikubwa kwa wananchi wote.
Sambamba na hayo, aliwataka wahitimu hao kujiendeleza zaidi, ili kuondosha changamoto zinazowakabili na kuendeleza kutoa huduma bora zaidi sambamba na kuzifahamu zinazowakabili watu wenye ulemavu wa uziwi.
Nae mwalimu wa mafunzo hayo, kutoka idara ya watu wenye ulemavu Zanzibar, Ibrahim Khamis Mwinyi, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kwa lengo la kuwasaidia jamii ya watu wenye ulemavu wa uziwi
Aidha alifahamisha kuwa mafunzo hayo ni ya awali na kusema kuwa wahitimu hao wanahitajika kuengeza nguvu ili kuweza kujifunza zaidi na kuweza kuwa wakalimani na kutoa huduma bora.
“Lugha ya alama ni sawa na lugha nyengine ikiwemo kiengereza au lugha nyengine ambayo ukiitaka itakutaka na endapo ukiiacha basi nayo itakuacha” alisema.