NA MARYAM HASSAN

ZOEZI la uhakiki kwa wastaafu lililokuwa likifanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (ZSSF) Unguja, limefikia tamati ambapo zaidi ya wanachama 8,328 wamehakikiwa katika wilaya ya Kaskazini na Kati.

Akitoa taarifa hizo ofisa Mwandamizi Masoko na Uhusiano kutoka (ZSSF) Raya Hamdan Khamis alisema zoezi hilo limekwenda vizuri kama walivyotarajia, ambapo mkoa wa Kaskazini wastaafu 677 walifanyiwa uhakiki wilaya ya Kati 374 na katika wilaya ya Kusini wanataraji kuwafanyia uhakiki wastaafu 400.

Ofisa huyo alisema wale ambao bado hawajafanikisha zoezi hilo wafike katika makao makuu ya ZSSF Kilimani ili kufanyiwa uhakiki ambao utawafanya kupata pencheni zao kwa uhakika.

Alifahamisha kuwa baada ya zoezi watafanya tathmini ya wastaafu ambao wamepata dharura ikiwemo maradhi ili nao kufuatiliwa katika makaazi yao kwa ajili ya kujiridhisha.

Alifahamisha kuwa katika zoezi hilo wastaafu wengi ni wanaume kuliko wanawake, kwa sababu ya utamaduni wa wazee wa zamani kuwapa nafasi kubwa ya elimu wanaume.

“Hili tunalielewa sote kuwa zamani mwanamke hakuwa na nafasi ya kufanya kazi kwa sababu anaonekana kuwa ni mama wa nyumbani tu ndio sababu hivi sasa tunawaona wanaume wengi lakini zama zijazo wanawake naamini nao watakuwa wengi” alisema.

Kuhusu kuongezewa pencheni wastaafu hao alisema zoezi hilo litafanyika kulingana na makusanyo yanayotokana na miradi iliyopo.

Miongoni mwa wastaafu walifika katika Halmashauri ya wilaya ya Kusini kwa lengo la kufanya uhakiki Hamida Haji ambae aliitumikia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar aliishauri (ZSSF) kuandaa utaratibu wa kuwafikia wazee hao vijijini mwao kwa lengo la kuwahakiki.

“Utaratibu waliouweka ni mzuri hakuna usumbufu yaani unakuja unaondoka tofauti na kipindi ambacho tukifuata huduma hizi Mjini ulikuwa ni usumbufu mkubwa” alisema.

Mohammed Ibrahim Simai alisema pencheni wanayopata haitoshelezi kujikimu kimaisha hivyo alishauri kuongezewa ili nao wapate kumudu hali ya maisha kwa sababu ya kupanda kwa bidhaa kila kukicha.

Alisema kwa kuwa ZSSF imeweka utaratibu wa kuwapatia pencheni kila mwezi nayo inasaidia kusukuma maisha mbele lakini nae aliomba kuongezewa kiwango cha fedha kwa sababu kiwango cha zamani cha mshahara na sasa viko tofauti jambo ambalo linawafanya kupata pencheni ndogo.