MNAMO Juni 29 mwaka huu mahakama kuu nchini Afrika Kusini ilimuhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo Jocob Zuma kutumikia kifungo cha miezi 15 kwa kushindwa kutii amri ya mahakama.

Ikiwa zaidi ya wiki moja sasa tangu mahakama hiyo itoe hukumu hiyo, rais huyo wa zamani ambaye anatakiwa ajisalimishe polisi ili apelekwe gerezani kuanza kifungo chake hajachukua hatua hiyo.

Kwa kinywa kipana akizungumza na waandishi wa habari Zuma alinukuliwa akisema kuwa hatajisalimisha polisi kufikia muda wa mwisho uliowekwa na mahakama, ambapo alipewa hadi usiku wa Julai 4 mwaka huu kujisalimisha mwenyewe.

Zuma aliyeagizwa kujisalimisha mwenyewe kwa polisi ili kuanza kifungo cha miezi 15 jela kwa kupuuza na kutoheshimu amri ya mahakama, amesema hatajisalimisha kufikia muda wa mwisho uliowekwa na korti.

Zuma aliwaambia waandishi wa habari katika makaazi yake yaliyopo Nkandla, wilaya ya Kwa-Zulu Natal kumbwa hakuna haja ya yeye kwenda jela na hukumu aliyopewa ya miezi 15 jela ni batili.

Aliwaeleza waandishi hao wa habari kwamba atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya kumpa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela pamoja na kuzuia agizo la kukamatwa kwake na polisi.

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 79, amesema kupelekwa jela wakati nchi hiyo ikipitia kwenye kilele cha janga la ugonjwa wa corona ni sawa na kuhukumiwa kifo.

Katika hatua nyengine Zuma aliwaambia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika nje ya makaazi yake ya Nkandla kuwa alinyimwa haki za kikatiba na majaji wa mahakama ya katiba nchini humo ilipomuhukumu kifungo cha miezi 15 jela.

“Siombi kuonewa huruma, lakini nataka haki. Umri wangu na hali yangu ya kiafya pamoja na mambo mengine hayakuzingatiwa wakati uamuzi ulipotolewa”, Zuma aliwaambia wafuasi wake hao.

Hivi sasa timu ya mawakili wake iliiandikia mahakama kudai kuwa hukumu dhidi yake ilikuwa na makosa, kwa nia ya aidha kupunguza kifungo hicho au kuifutilia mbali hukumu yenyewe.

Zuma, aliongoza wafuasi wake kuimba wimbo maarufu wakati wa enzi za kupambana na ubaguzi wa rangi wa “Umshini Wami” ukimaanisha niletee bunduki yangu, wimbo ambao amekuwa akiitumia sana katika mikutano yake ya siasa chini humo.

Huku Zuma akipinga kujisalimisha kwa polisi wafuasi wake wamepiga kambi katika makaazi yake wakitengeneza kile wanachokiita ngao ya binadamu ili kuzuia kiongozi huyo asikamatwe.

“Tuko hapa kumlinda Jacob Zuma asikamatwe. Yeyote anayetaka kumkamata lazima atukamate sisi kwanza, ndio maana tuko hapa. Wakija hapa, tukawepo hapa. Hata kama itachukua mwaka mzima, watatukuta hapa. Tutazuia mtu yeyote atakayejaribu kumkamata msholozi mbele yetu”, alisema.

Mfuasi wake mmoja, Lindokuhle Maphalala, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kama mkuu wa polisi angekuja kumkamata Zuma “kwanza inabidi aanze na sisi.”

Wafuasi hao wameapa kusababisha vurugu na kukwamisha oparesheni za serikali iwapo Zuma atafungwa na kuapa kumlinda Zuma, wafuasi hao wamemtaka Rais Cyril Ramaphosa aachie madaraka.

Hata hivyo, mkusanyiko huo wa wafuasi wa Zuma ni haramu kwa kuwa unavunja kanuni za kudhibiti ugonjwa wa corona, lakini hakukuwa na askari waliokwenda kuwaondosha watu.

Baadhi ya watu nchini humo hasa mashirika ya kupigania haki yameeleza kuwa hali hiyo wanaitafsiri kuwa kiongozi huyo wa zamani yupo juu ya sheria kwa kuwa ana nguvu kubwa ya kisiasa.

Mnamo Julai 3 mwaka huu mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini ilikubali kusikiliza ombi la Zuma la kutaka kifungo cha miezi 15 jela kifutiliwe mbali.

Haijulikani kama uamuzi wa mahakama wa kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wake wenyewe utaathiri siku ya mwisho iliyowekwa ya Zuma kujisalimisha.

Mahakama ya katiba ilisema kwamba ilipokea ombi la kukata rufaa la Zuma na italifanyia maamuzi ya ombi hilo mnamo Julai 12.

Wakati huo huo, taasisi ya Jacob Zuma, mfuko wa misaada wa rais wa zamani, ilisema rufaa dhidi ya amri ya kukamatwa itasikilizwa na mahakama kuu ya jimbo la KwaZulu-Natal.

Zuma 79 aliondolewa madarakani mnamo mwaka 2018, baada ya miaka tisa madarakani, akikabiliwa na shutuma za ufisadi, ambapo anakabiliwa na shutuma za kutubia vibaya madaraka yake.

Hata hivyo, Zuma amerudia kusema kuwa yeye ndiye muathirika wa njama za kisiasa na amekataa pia kutoa ushirikiano katika uchunguzi juu ya makosa wakati wa uongozi wake.

Rais huyo wa zamani alitoa ushahidi mara moja tu wakati wa uchunguzi wa kile kilichojulikana kama kutekwa kwa serikali lakini akakataa kujitokeza tena baadaye.

Katika suala tofauti la kisheria, Zuma alikana shutuma zilizomkabili katika kesi yake ya ufisadi iliyohusisha makubaliano ya silaha ya thamani ya dola bilioni 5 kutoka miaka ya 1990.

Mvutano wa kisiasa umekuwa ukiongezeka nchini Afrika Kusini, huku wanachama wa chama cha maveterani wa jeshi wakitishia kwamba nchi hiyo italegalega endapo Zuma atakamatwa na kupelekwa jela.

Chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, ambacho Zuma alikuwa akiongoza, kimetaka utulivu, lakini akiogopa mgongano mkutano wa kamati yake kuu ya kitaifa umeahirishwa.