ALGIERS, ALGERIA

ALGERIA imelituhumu kundi linaloliita la kigaidi na kudai linasaidiwa na Morocco na Israel, kuanzisha moto wa msituni uliouwa watu 90 mwezi huu na kusababisha hasara kubwa ya mali.

Ofisi ya rais wa nchi hiyo ilisema watu 22 wamekamatwa kuhusiana na moto huo, na kuongeza kuwa lawama zote inalibebesha kundi la Islamic Ramash na MAK la watu wanaozungumza lugha ya Amazigh katika jimbo la Kabylie.

Aidha, ofisi ya Rais Abdelmadjid Tebboune ilisema inatafakari upya uhusiano wake na Morocco baada ya kikao maalumu cha kamati ya usalama wa taifa kilichoongozwa na rais huyo. Tangazo la ofisi hiyo limesema usalama utaimarishwa katika mpaka wa magharibi unaozitenganisha Algeria na Morocco.

Uhusiano baina ya nchi hizo ulizorota zaidi mwezi uliopita, baada ya mwanadiplomasia wa Morocco mjini New York kusema watu wa jimbo la Kabylie wanayo haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe.