ALGIERS, ALGERIA

WAZIRI wa Mambo ya nchi za nje wa Algeria Ramtane Lamamra amesema nchi hiyo imekata uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco.

Alisema kuwa, Morocco imehusika na moto uliochoma misuti ya Algeria katika siku za karibuni na kwamba Algiers imeamua kukata uhusino wake na Rabat.

Siku chache zilizopita Algeria iliuhusisha moto mbaya uliotokea hivi karibuni nchini humo na makundi mawili ambayo imeyatambua kuwa ni magenge ya kigaidi, na kusema kuwa moja ya kati ya makundi hayo liliungwa mkono na kufadhiliwa na Morocco na Israeli.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Algeria alisema nchi hiyo pia itaendeleza jitihada katika Umoja wa Afrika za kufutwa hadhi ya mwanachama mwangalizi iliopewa utawala wa Israel.

Uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat wa kuipatia Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika AU umezusha utata mkubwa baina ya nchi za Afrika.

Nchi 13 wanachama wa Umoja wa Afrika zilitangaza rasmi kuwa zinataka uamuzi wa kuipa Israel hadhi ya mwangalizi katika umoja huo ubatilishwe ili kulinda heshima na nafasi ya Umoja wa Afrika.