Alitamba Small Simba, Miembeni, timu za taifa
Azishauri klabu kutafuta wafadhili binafsi.
ZASPOTI
“SOKA ni mchezo niliokuwa naupenda kwenye damu yangu na sijarithi kutoka katika familia yangu kwa vile hakuna mtu katika familia yangu aliyekuwa mwanasoka”.
Hayo ni maneno ya mlinda mlango maarufu aliyeng’ara katika visiwa vya Zanzibar na hata katika nchi za Falme za Kiarabu, Ali Muhsin Abeid.
Mlinda mlango huyo alifanikiwa kujizolea sifa nyingi kutokana na mapenzi na ari ya mchezo huo unaopendwa na mashabiki wengi duniani.
Kama utataja majina ya wachezaji au walinda mlango waliotamba hapa visiwani kuanzia mwaka 1980,hutoweza kukamilisha majina hayo kama hutomtaja Ali Muhsin.
Kutokana na historia nzuri aliyonayo katika soka la Zanzibar, nililazimika kumtafuta nyota huyo na kufanikiwa kukutana nae hapo nyumbani anapoishi katika maeneo ya Michenzani na kuzungumza nae juu ya alivyoanzia soka na alipofikia hadi kustaafu.
Kama ilivyo kawaida ya wachezaji wengi wa mchezo huo akiwa mdogo, Ali Muhsin, alianza kucheza mpira akiwa mdogo wakati anakaa katika mtaa wa Mkamasini mjini Unguja.
Anasema alianza kucheza soka katika timu ya Shangani na baadae alijiunga na Mchangani kabla ya kuhamia Small Simba ambapo timu hizo alicheza daraja la Juvenile.
Anasema, akiwa Small Simba ilikuwa ikinolewa na kocha, Khelef Khamis ambaye aliiwezesha kuipandisha daraja la Central mwaka 1978.
“Nilianza timu ndogo ndogo za mitaani lakini baadae nikajiunga na Small Simba mpaka tukafika daraja la Central”.
Anasema, mwaka 1981 kikosi cha Small Simba kilipata nafasi ya kwenda Tanga wakiwa chini ya mwalimu Abdulghan Himid Msoma ambapo alifanya mazungumzo na uongozi wa Coastal Union, kwa lengo la kufungua ukurasa wa mafanikio kwa klabu hiyo.
“Uongozi wa Coastal Union ulimshauri kocha Msoma kuipeleka timu yake ya kikosi cha kwanza,”alifafanua.
Kutokana na kiwango kizuri walichokionesha uwanjani Small Simba iliweza kupata nafasi ya kucheza daraja la pili pamoja na timu nyengine.
Alizitaja timu hizo ni pamoja na Nyuki, Shangani, Black Fighter, ambapo mwaka 1982 Small Simba ilifanikiwa kupata nafasi ya kucheza ligi kuu ya Zanzibar.
Anasema mwaka 1983 kikosi hicho kilitamba ndani ya visiwa hivi na kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Zanzibar wakati huo mashabiki wakiita jina la ‘Moto Small’.
Mlinda mlango huyo, anasema, akiwa ndani ya kikosi hicho kilichotwaa ubingwa huo, alikutana na wanandinga wengi akiwemo Salum Bausi, Abdulwakati Juma, Muhidin Siso,Hussein Ngulungu na wengine wengi.
Anasema, mwaka 1985 ilifanikiwa kutwaa tena ubingwa wa Zanzibar uliotemwa na KMKM.
Anasema kutokana na umahiri wake akiwa mlangoni, mwaka 1983 alichaguliwa kujiunga na timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’.
Alisema kutokana na sababu mbali mbali alilazimika kukihama kikosi cha Small Simba mwaka 1986 na kujiunga na klabu ya Miembeni .
Akiwa katika timu ya Miembeni alikutana na wachezaji mbali mbali mahiri akiwemo Mcha Khamis, Ahmed Kibapa, Kibwana Makungu na wengine wengi.
“Nilihama Small Simba baada ya kuletwa James Kisaka wakati nikiamini ndiye mlinda mlango nambari moja huku nikiwekwa benchi nikaamua nijiunge na Miembeni”, alisema.
Kipaji alichokua nacho Ali Muhsin wakati huo, kilivuka hadi nje ya mipaka ya Zanzibar ambapo kwa umahiri wake ulimfanya achaguliwe katika kikosi cha taifa Tanzania ‘ Taifa Stars’ mwaka 1987.
“Huko niliungana na Othman Abadallah ‘Forman’ ,Nassor Bwanga, Ramadhan Leny, Madaraka Suleiman,Abeid Mziba na wengine wengi,”.
“Namshkuru Mungu nilipata nafasi ya kuichezea timu ya taifa Tanzania na timu ya taifa ya Zanzibar na kote huko nilikutana na wachezaji wengi mahiri na nikajifunza mengi kutoka kwao,”aliongezea.
Mwaka 1988, Ali Muhsin alipata nafasi ya kwenda nchini Oman katika mji wa Surri na kujiunga na timu ya Talia ambayo ilikua ikicheza ligi ya kanda nchini humo.
Anasema katika timu ya Talia alidumu nayo kwa miaka minane na baadae alirudi nyumbani na kujiunga na timu ya National iliyokuwa ikinolewa na marehemu Abdulnabi Hassan Tesso ambapo alikaa kwenye kikosi hicho kwa mwaka mmoja na baadae kuachana na mchezo wa soka.
“Niliamua kuachana na kucheza mpira kutokana na wenzangu wengi tuliokuwa tukicheza soka pamoja walikuwa wameshaacha nikaona na mimi hakuna haja ya kubakia uwanjani ingawa nilikua bado sijamalizika kisoka,”alisema.
Ali Muhsin kwa umbile la nje ni mrefu mwenye rangi ya maji ya kunde,mcheshi na mpenda utani, alisema katika mchezo wa soka aliweza kukumbana na matatizo mengi ikiwemo fitna za kisoka lakini aliweza kutatua mwenyewe matatizo hayo.
Kwa upande wa faida, anasema ni pamoja na kujijenga kiafya kwa kufanya mazoezi,kupata umaarufu na kutembea sehemu mbali mbali .
Alizitaja nchi ambazo alitembea wakati akiwa mchezaji ni pamoja na Kenya, Madagascar, Zambia, Uganda na Malawi.
“Faida zipo nyingi, lakini, sio kujenga nyumba wala kufanya jambo lolote la maana”,alisema.