ADDIS ABABA, ETHIOPIA

DAWATI  la kupambana na ugaidi na mambo ya katiba la Mahakama Kuu ya Ethiopia limemhukumu kifungo cha maisha jela Tilahun Yami ambaye ni muuaji wa mwanamuziki maarufu Hachalu Hundessa.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Fana (FBC), Hundessa ambaye ni mwanamuziki aliyeshughulikia haki za watu wa kabila la Oromo, alipigwa risasi na kufa Juni mwaka jana.

Mahakama hiyo pia iliwahukumu washirika wa Yami, Kebede Gemechu kifungo cha miaka 18 jela na Abdi Alemayehu kifungo cha miezi sita.

Hata hivyo hadi sasa haijaelezwa sababu ya mwanamuziki huyo kuuawa.

Mauaji ya Hundessa yalisababisha vurugu kubwa mjini Addis Ababa na mkoa wa Oromia na kupelekea watu zaidi ya 200 kuuawa.