ZASPOTI
RAIS wa Rwanda, Paul Kagame ambaye ni shabiki wa Arsenal, ameelezea kughadhabishwa kwake na miamba hiyo kufungwa na klabu mpya iliyopanda daraja katika mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu ya England.
Brentford, iliyorejea katika ligi hiyo baada ya miaka 74, iliichabanga Arsenal magoli 2-1.

Kagame mara kwa mara huwaangalia washika bunduki hao, klabu ambayo serikali yake iliifadhili.
Baada ya mechi hiyo aliandika katika mtandao wake wa Twitter: “Hatupaswi tu kutoa udhuru au kukubali upuzi. Timu lazima iiundwe kwa lengo la kushinda na kushinda”.
Katika ujumbe mwengine alitaka wawe na mpango utakaozaa matunda na kulalamika kwamba mashabiki hawahitaji kuzoea hali hii.

Tangu mwaka 2018, serikali ya Rwanda imekuwa na makubaliano ya udhamini yenye utata ya thamani ya zaidi ya pauni milioni 30, ambayo inajumuisha nembo ya ‘Tembelea Rwanda’ inaoonyeshwa kwenye mikono ya fulana ya Arsenal.

Wakosoaji wamesema ni mfano wa kiongozi wa kimabavu wa nchi masikini ya Kiafrika inayofadhili klabu tajiri ya soka. Lakini, serikali ya Rwanda inasema udhamini huo zaidi unajilipa kupitia mapato ya utalii.
Wakati huo huo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alielezea kushangazwa na wachezaji wake kufuatia kufuatia kipigo hicho.

Arsenal ambayo kwa misimu kadhaa sasa imekuwa na mwendo wa kusua sua kwenye ligi hiyo na kupelekea kukosa kucheza michuano ya Ulaya.
Washika mtutu hao wa London walikuwa bila ya huduma ya nahodha, Pierre-Emerick Aubameyang pamoja na mshambuliaji, Alexandre Lacazette, lakini, ingizo jipya, Ben White kutoka Brighton alikuwa sehemu ya mchezo. (BBC Sports).