NA SABRA MAKAME, SCCM

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa China kuimarisha barabara kwa kujenga njia za waenda kwa miguu na mitaro kuptishia maji ya mvuaj katika barabara ya Kiembesamaki hadi Mtoni (Mkapa road).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Jamal Kassim Ali, alieleza hayo alipofanya ziara ya kukagua  barabara mbali mbali kuanzia Kiembesamaki, Kwa Mchina Mwanzo, Daraja bovu na Jang’ombe, mkoa wa Mjini Magharibi.

Waziri Jamali alisema kazi hiyo itafanyika kutokana na fedha za msaada wa shilingi bilioni 14.7 za kitanzania ambazo serikali ya China iliahidi kuipatia Zanzibar mwanzani mwa mwaka huu ikiwa ni sehemu ya misaada ya nchi hiyo kwa Tanzania.

“Mwezi Machi mwaka huu tulisaini msaada wa fedha kutoka chana na serikali ilipanga kuona namna gani tunaendeleza barabara iliyoanzia Kiembesamaki hadi Mtoni ambayo barabara ina urefu wa kilomita 8,” alisema Jamal.

Akiwa katika ziara hiyo Jamali alisema lengo kuu la matengenezo hayo ni kuongeza uimara ya wa barabara hiyo lakini pia kuweka mandhari mazuri na usalama kwa watu wanaotembea barabarani.

Alisema katika ziara hiyo aliambatana na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar ili kumuonesha umuhimu wa mradi huo pamoja na kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa haraka ili kuhakikisha kazi iliyokusudiwa inafanyika kwa wakati.

Vile vile Jamali alisema katika ziara hiyo Balozi huyo amejiridhisha na ameahidi kuwa fedha za mradi huo zinapatikana kwa haraka.

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali, alisema ziara hiyo imejumuisha wizara mbili ikiwemo Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na wizara ya nchi, Ofisi ya Raisi,Fedha na Mipango ili kuja na mpango wa pamoja wa utekelezaji wa mradi huo.

“Barabara hii bado haipo katika hali nzuri, tunatarajia kuiimarisha kama ilivo barabara ya Uwanja wa Ndege ambayo inaendelea na ujenzi,” alieleza Waziri Rahma.

Alieleza kuwa wizara hizo zimeona hajaya kuanza maandalizi ya mradi huo kabla ya kumaliza kazi katika barabara ya uwanja wa ndege.