NA ABOUD MAHMOUD
VIJANA nchini wametakiwa kuwa na mwamko katika suala zima la kudumisha usafi wa mazingira katika maeneo yao, ili kwenda sambamba na kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi ya kuuweka mji safi.
Kauli hiyo, imetolewa na Mkuu wa Idara ya mazingira Baraza la mji Kati, Khamis Ali Kawambwa, wakati akikabidhi vifaa vya usafi kwa kikundi Cha usafi wa mazingira Shehia ya Tunguu.
Alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anadumisha usafi katika eneo analoishi, ili kujiepusha na maradhi mbali mbali yanayosababishwa na uchafu .
“Nakuombeni wananchi wote kuhakikisha tunakwenda sambamba na kauli ya Rais wetu, Dk. Mwinyi, ambayo kila siku anaizungumzia kuhusiana na kudumisha usafi katika maeneo yetu,”alisema .
“Nakuombeni wananchi wenzangu kuhakikisha tunavitunza vifaa vyetu hivi na kuvitumia kama ilivyokusudiwa ili twende sambamba na dhamira ya kudumisha usafi katika maeneo yetu,”alifahamisha.
Nao vijana wa kikundi cha usafi wa mazingira wa Shehia ya Tunguu wamesema watahakikisha wanavitumia vifaa hivyo Kama ilivyokusudiwa, jambo ambalo litachangia kuibadilisha shehia hiyo katika suala zima la usafi wa mazingira.