KABUL, AFGHANISTAN

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha dharura kujadili hali nchini Afghanistan baada ya Wataliban kuukamata mji mkuu wa nchi hiyo, Kabu.

Kikao hicho cha hadhara ambacho kitafuatiwa na chengine cha faragha vilipendekezwa na Estonia pamoja na Norway.

Ofisi ya Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres ilisema kiongozi huyo anafuatilia yanayojiri Afghanistan kwa wasiwasi mkubwa, na anawahimiza Wataliban na pande zote zinazohusika kuchukua kila tahadhari katika kuyalinda maisha ya watu na kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji ya kibinadamu.

Ripoti kutoka Afghanistan zinasema kuwa Wataliban wamechukua udhibiti kamili wa serikali, baada ya aliyekuwa rais, Ashraf Ghani kuikimbia nchi.

Marekani imeondoka katika ubalozi wake mjini Kabul na kuwahamishia raia wake katika uwanja wa ndege ambao sasa imeuweka chini ya ulinzi wake. Ujerumani pia imewaondoa raia wake kutoka Afghanistan.