NA ASHURA SLIM, CHUO KIKUU HURIA
BARAZA la Wauguzi na Wakunga Zanzibar, limejipanga vyema katika kuhakikisha wauguzi na wakunga wanatoa huduma bora na kwa wakati stahiki bila ya malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi.
Kufuatia kongamano la wauguzi la Julai 27, 2021 juu ya tathmini ya utendaji kazi pamoja na kuibua kero mbali mbali zinazo wakabili wauguzi pamoja na wananchi.
Akizungumza na Zanzibar Leo, Mrajis wa Baraza hilo, Vuai Kombo Haji, amesema hawatomvumilia muuguzi yoyote atakae thibitika kuwanyanyasa wagonjwa kwa kuwatolea maneno ya kashfa, kwani kitendo hicho ni kimyume na maadili ya fani hiyo.
Alisema Muuguzi yoyote atakae kwenda kinyume cha sheria na anachukuliwa hatua bila ya kumtizama machoni, kwa hospitali za serikali na binafsi, wao ndio wasimamizi wakubwa.
Pia amewataka wananchi kuyafata maagizo ya serikali ikiwemo ya kuvitumia vituo vya afya viliopo katika maeneo yao, ili kuepuka msongomano katika Hospitali ya Mnazimmoja hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa corona.
Hatua hiyo, itasaidia kuwapunguzia mzigo wauguzi hao, ili kuwawezesha kutoa huduma kwa weledi na wakati.
Akizungumzia changamoto wanazo kumbana nazo alisema ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi, idadi ndogo ya wauguzi, kutokupandishwa kwa madaraja pamoja na maslahi madogo ya wafanya kazi.
Hata hivyo, Mrajis huyo kuhusu wauguzi waliopata ajali ya Shiyanga wakitokea masomoni Uganda Chuo cha Bugema alisema Wizara hiyo itahakikisha majeruhi hao wanamaliza masomo yao vizuri, na wanaendelea kufuatilia afya zao watakua nao pamoja kwa kila hatua.