BEIRUT, LEBANON
BEI ya mafuta nchini Lebanon imeongezeka kwa asilimia 70 hadi kufikia Jumapili baada ya kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, na kuzidisha shinikizo zaidi katika taifa hilo ambalo linakabiliwa na mzozo mbaya wa kiuchumi.
Gharama ya mafuta sasa imeongezeka mara tatu zaidi katika muda wa miezi miwili baada ya benki kuu kupunguza msaada wake kwa uagizaji wa bidhaa muhimu.
Uhaba mkubwa wa mafuta umesababisha watu nchini humo kutafuta njia mbadala za kufika katika sehemu zao za kazi badala ya kutumia magari.
Foleni ndefu za waendesha magari zimeshuhudiwa katika vituo ya mafuta ambavyo bado viko wazi.
Kiongozi wa vuguvugu la waislamu wa dhehebu la Kishia la Hezbollah ameahidi kuwa mafuta zaidi kutoka Iran yatawasili hivi karibuni nchini humo ili kusaidia kutatua uhaba mkubwa wa mafuta.