WASHINGTON, MAREKANI

RAIS wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett wamefanya mkutano wa kwanza wa ana kwa ana mjini Washington.

Kwenye ziara hiyo ya kwanza nchini Marekani tangu awe waziri Mkuu, Bennett anatarajiwa kumshinikiza Biden kuachana na azma yake ya kufufua mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Kabla ya kuanza safari kwenda Washington, Bennett aliweka wazi dhamira yake kuu kuzuru Marekani kuwa ni kumrai Biden kutoirudisha Marekani katika mkataba wa nyuklia, akidai tayari Iran imepiga hatua katika kurutubisha madini ya urani na kuregeza vikwazo kutaipa Iran rasilimali zaidi kuwaunga mkono wapinzani wa Israel katika kanda hiyo.

Bennett alikutana tofauti na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony Blinken pamoja na waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin kujadili masuala kuhusu Iran.

Biden aliweka wazi nia yake kutaka kunusuru mkataba huo wa kihistoria ulioafikiwa mwaka 2015 chini ya rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama ambapo rais wa zamani Donald Trump alipuuza na kuiondoa nchi yake mnamo mwaka 2018.