ZANZIBAR kama zilivyo nchini nyengine za visiwa inatekeleza mikakati mbalimbali katika kuhakikisha inaongeza pato la taifa, hasa kwenye makusanyo ya fedha za kigeni.
Ukiachilia utalii sehemu nyengine muhimu sana ambayo inaweza kuwa tegemeo la uchumi wa Zanzibar ni ukulima wa bidhaa za viungo ambazo zinazalishwa katika maeneo mbalimbali.
Bidhaa kama hiliki, mdalasini, vitunguu thomu, pilipilimanga, kungumanga, tangawizi, karafuu na nyenginezo kwa wananchi wengi wa Zanzibar wanachukulia kwenye matumizi ya kawaida.
Tofauti tunavyoyachulia matumizi ya bidhaa hizo hapa kwetu, katika nchi za wenzetu bidhaa za viungo zinauzwa kwa bei ya juu na ni adimu sana kupatikana kwenye masoko.
Tunadhani hii ni fursa muhimu ambayo inaweza kuwatoa vijana wetu kiuchumi na kujipatia kipato hasa wale wanaoishi katika maeneo ambayo bidhaa za viungo zinastawi sana.
Lazima tukiri kwamba vijana wetu wengi hawajatanabahi thamani ya maisha wanayoweza kuyapata endapo watajiingiza kwenye ukulimwa wa bidhaa za viungo.
Tuna tatizo kubwa hivi sasa hapa Zanzibar vijana wengi kukimbilia mijini wakihaha kutafuta ajira na kwamba ajira hizo hawazipati na kuishia kwenye vitendo viovu.
Hivyo, kuwepo kwa soko la uhakika bila shaka kutaweza kuwashawishi vijana wa namna hii waache ndoto za kuhamia mijini na badala yake washike majembe kuelekea mashambani kulima bidhaa za viungo.
Bidhaa za viungo za Zanzibar lazima ziwe na thamani kwenye soko lolote duniani kwa sababu zinalimwa katika mazingira asilia na kwamba hazizalishwi kwa kutumia kemikali.
Bidhaa za namna hii ndizo zenye thamani kwenye masoko duniani, hivyo tunaamini kama vijana watashajiishwa kikamilifu na masoko ya uhakika yatakuwepo, hakuna sababu ya kijana kukimbilia mji wakati fedha za uhakika zipo kijijini.
Kwa wale wasio fahamu ni kwamba bidhaa kama vile pilipili manga, karafuu, tangawizi, mdalasini na nyenginezo ni tiba ya maradhi mbalimbali yanayotuandama katika maisha yetu ya kila siku.
Bila ya hata kujua, wakati mwengine bidhaa hizo unapozitumia zinaweza kuwa kinga na tiba ya maradhi makubwa, ambayo pengine yangeweza kukugharimu mamilioni ya fedha kama ungekwenda hospitali.
Katika kuziingiza kwenye soko la kimataifa bidhaa zetu za viungo, lazima yawepo maandalizi kwa wakulima na wafanyabishara wetu, ili bidhaa hizo ziweze kumudu ushindani.