NA YUSSUF ALI (WAMM)

BODI ya Wakala wa Majengo Zanzibar, imetakiwa kutekeleza kazi zake kwa kuzingatia usimamizi na ufuatiliaji wa majukumu na miongozo iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kufanya hivyo, kutawezesha bodi hiyo kutekeleza majukumu hayo kwa urahisi na ufanisi ulio bora na kuondokana na changamoto zitakazoweza kujitokeza.

Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amebainisha hayo huko ofisini kwake Maisara wakati alipokutana na uongozi wa bodi hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Msanifu Haji Mussa, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa kazi mbali mbali zinazohusiana na bodi hiyo.

Waziri amefahamisha kua  moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kuishauri Serikali katika suala zima la ujenzi  wenye kuzingatia viwango vya ubora wa nyumba za kisasa hapa nchini, pamoja na kusimamia na kuzifatilia nyumba za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha ameitaka bodi hiyo kujipanga vizuri katika kupanga mji wa serikali kwa kujenga majengo ya Mawizara na Taasisi za Serikali ili kuboresha haiba ya jiji la Zanzibar.

Wakati huo huo, Waziri Pembe, ameitaka wakala wa majengo kuzifatilia na kuziorosha nyumba zote za Serikali  Unguja na Pemba, na kuwaangalia kwa watumiaji wa nyumba hizo kama wana sifa za kuendelea kuishi katika nyumba au wamemaliza mda wao kwa kufuata sheria zilizowekwa.

Aidha, Pembe alisisitiza haja kwa wakala wa majengo kujiengeza kitaalamu katika kubuni njia za uanzishwaji wa ujenzi wa nyumba za kibiashara kufanya hivyo kutapelekea kuongeza pato la serikali na wananchi wataweza kunufaika kupitia mpango huo.

Bodi ya wakala wa majengo yenye wajumbe saba imeanzishwa kwa lengo la kuisaidia Serikali katika kutoa ushauri wa kitaalamu unaohusiana na suala zima la ujenzi wa nyumba za kisasa unaozingatia viwango vya kimataifa ili kuleta mabadiliko nchini.