BRASILIA, BRAZIL

MAGAVANA wa majimbo nchini Brazil wameonyesha wasiwasi wao juu ya hatua ya jeshi la polisi kumuunga mkono Rais Jair Bolsonaro.

Wasiwasi wao unafuatia mkutano wa magavana mjini Brasilia mapema wiki hii ambapo walijadili juu ya mgogoro wa kisiasa nchini humo wakati Rais Bolsonaro akionyesha dalili za wazi za kuipinga mihimili ya utawala, na kuishambulia tume ya uchaguzi nchini humo.

Kati ya magavana 27 wa Brazil, 25 walionyesha wasiwasi wao juu ya hatua ya polisi wapatao 500,000 kumuunga mkono Rais Bolsonaro kuelekea kwa uchaguzi mkuu ujao.

Sheria nchini Brazil zinawazuia polisi kushiriki maandamano ya kisiasa, lakini wengi wao wanatarajiwa kujitokeza kwenye maandamano ya Septemba 7 ya kumuunga mkono Bolsonaro.

Kura za maoni zinaonyesha kuwa Rais wa zamani mwenye kuegemea siasa za mrengo wa kushoto Luis Inacio Lula da Silva ana umaarufu mkubwa wa kisiasa, wakati wakosoaji wakisema huenda Bolsonaro akayapinga matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.