ZASPOTI
BRITNEY Spears ni jina lililojipatia umaarufu mkubwa nchini Marekani na duniani kwa ujumla kupitia tasnia ya muziki, ambapo ameporomosha vibao kadhaa vilivyoshika chati kwa nyakati tofauti.
Moja ya wimbo mzuri ulioporomoshwa na mwanamzuki huyo aliupa jina la “I was born to make you happy”, kwa maana ya ‘nimezaliwa ili kukufanya uwe na furaha’, sijui Britney alikuwa akimuambia nani maneno hayo.
Mwanadada huyo mrembo kiasi mkali wa miondoko ya pop na hata kwenye uizaji wa filamu, alizaliwa Disemba 2 mwaka 1981 katika mji wa McComb uliopo katika jimbo la Mississippi.
Hata hivyo alikulia katika mji wa Kentwood, Louisiana ambapo akiwa mdogo alionekana kwenye majukwaa akiigiza tamthilia na kwenye televisheni kabla ya kuingia mkataba na Jive Records mwaka 1997.
Albamu zake za kwanza mbili ‘Baby One more Time’ ya mwaka 1999 na ‘Oops!..I Did It Again’ ya mwaka 2000 zilimpa mafanikio makubwa katika soko la muziki ulimwenguni.
Makala hii haina nia ya kuangazia kwenye maisha ya muziki na filamu ya Britney, bali inataka kukupa kitu ambacho hukuwa ukikijua ama pengine pia hujawahi kukisikia hasa kuhusu mali zake.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, Britney ana utajiri unaofikia dola milioni 60 ambao unatokana na harakati zake anazozifanya kwa nyakati mbalimbali ikiwemo muziki, uigizaji na hata biashara.
Kitu ambacho pengine hukuwa ukikifahamu ni kwamba kwa takariban miaka 12 iliyopita hadi mwezi Julai, mwaka 2021 udhibiti wa mali za mwanamuziki huyo ikiwemo hadi matumizi yake binafsi ya fedha alizozichuma kwa mikono, nguvu na jasho lake zilikuwa chini ya udhibiti wa baba yake, Jamie Spears.
Unaweza kujiuliza kwanini mali za Britney zilikuwa chini ya uangalizi wa baba yake? Hali hiyo ilitokana na kwamba mnamo mwaka 2007 baada ya kutalakiana rasmi na aliyekuwa mumewe Kevin Federline, alikubwa na matatizo ya akili hali hiyo ilisababisha kupoteza haki ya kutunza watoto wake wawili.
Ilidaiwa baada ya kuingia kwenye matatizo ya ndoa na kuishia kuachana na mumewe, Britney aliingia kwenye matatizo ya msongo wa mawazo na kuanza kutokuwa sawa kiakili.
Mambo aliyokuwa akiyafanya hayakuwa ya kawaida na watu wengi walimuona kama kituko pale alipojitokeza hadharani akiwa amenyoa nywele zake.
Tukio hilo liligonga vichwa vya habari nchini Marekani ambapo pia aligonga vichwa vya habari alipopiga gari la aliowashuku wanahabari wa udaku kwa mwamvuli, baada ya kubaini kwamba wanataka kumpiga picha.
Kutokana na kufanya mambo yasiyo ya kawaida, Britney alipelekwa katika kituo cha huduma cha kurekebisha tabia mara kadhaa, pia alianza kupewa matibabu ya afya ya akili baada ya kukataa kuachia vijana wake katika mgogoro na polisi.
Mnamo mwaka 2008 baada ya baba yake mzee Jamie Spears kumuona mwanawe yuko katika hali hiyo aliiomba mahakama iridhie jukumu la kutunza mali zake ikiwemo kitita kikubwa cha fedha.
Hali hiyo hutokea kwa mahakama kuwa na nguvu dhidi ya watu ambao hawawezi kufanya maamuzi yao wenyewe, iwapo watawekwa katika kundi la wenye ugonjwa wa akili wa ‘dementia’ au matatizo mengine ya akili.
Chini ya makubaliano ya kisheria, Spears hajadhibiti mali zake zote ikiwemo fedha na hata kazi zake za muziki tangu uamuzi huo ulipotolewa mwaka 2008.
Badala yake, baba yake na mawakili wake wamekuwa na nguvu ya kumfanyia maamuzi kuhusu maisha yake ya kibinafsi. Pia matumizi yake ya kifedha ni lazima yarekodiwe mahakamani.
Hadi kufikia mwaka 2018, inasemekana Spears alikuwa na utajiri wa dola milioni 59 kulingana na tovuti ya masuala ya fedha ya Marekani, Business Insider.
Mwaka huo huo, Spears alitumia dola milioni 1.1 kama ada ya kisheria, kulingana na nyaraka za mahakama zilizoangaziwa na tovuti ya Entertainment Tonight.
Pamoja na mahakama kukubali kutokana na sababu za afya ya akili ya mwanamuziki huyo kwa wakati huo, Britney alipopata ahuweni aliendelea na shughuli zake kama kawaida kwani alitoa albamu tatu na kujitokeza katika vipindi vya televisheni mara kadhaa vilivyozidi kumuingizia fedha.
Mnamo mwaka 2020 baada ya Britney kupona msongo wa mawazo na matatizo ya akili, aliona umefika wakati jukumu la baba yake kudhibiti mali zake ikiwemo fedha lirudi kwenye mamlaka yake.
Britney alifungua kesi kuiomba mahakama imrejeshee mamlaka ya kumiliki fedha zake na iondoshe uwezo wa baba yake kuwa na nguvu za umiliki wa mali.
Hatimaye hivi karibuni baba yake Britney Spears amekubali kuacha jukumu la kudhibiti mali za binti yake baada ya zaidi ya miaka 12, taarifa za vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.
Mwanamuziki huyo baada ya kupona alifikiria kumuondoa baba yake katika jukumu hilo na kutaka ashtakiwe kwa kutumia vibaya mali zake.
Mara zote, Jamie Spears amekuwa akikanusha madai ya kutumia vibaya mali za mwanawe hasa fedha na kueleza wasiwasi wake juu ya hali ya afya ya akili ya mwanawe.
Huku kampeni ya kupinga udhibiti wa mali ya Britney ilianzishwa na baadhi ya mashabiki na kuitwa #FreeBritney, ambapo wanaamini kuwa maisha ya mwanamuziki huyo na taaluma yake yanadhibitiwa kinyume na matakwa yake.
Kesi hiyo ambayo ilichukua muda kumalizika ilipata sura mpya baada ya kuzinduliwa kwa Makala ya Framing Britney Spears ambayo imeangazia mzozo wa usimamizi wa mali za muimbaji huyo.
Mwanamuziki huyo mwenye miaka 39, alimwambia hakimu kuwa akilazimishwa kufanya maonesho bila ridhaa yake na kuzuiwa kuwa na watoto.
Usimamizi wa kisheria wa Spears umegawanyika katika sehemu mbili, upande mmoja ni kwenye nyumba zake na masuala ya kifedha na upande mwIngine ni kwake kama mtu.
Mwaka 2019, baba yake alijiondoa katika usimamizi wa masuala binafsi ya binti yake kutokana na masuala ya kiafya lakini mwimbaji huyo aliandika barua kuomba baba yake aondolewe kwenye udhibiti wa mali zake.
Baadae akasema hataimba kwenye majukwaa tena kama baba yake ataendelea kubaki katika jukumu hilo la udhibiti wa mali zake.
Akijibiwa maombi yake, wakili wa Spears alisema kuwa nakala za mahakama hazitoi muongozo wa kujiondoa.
Wakati wakili wa mwanamuziki huyo, Mathew Rosengart, alitoa taarifa inayosema: “Huu ni ushindi mkubwa kwa Britney Spears na hii ni hatua nyingine katika kupata haki.”