NA KASSIM ABDI, OMPR

VIONGOZI na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mjini wameiomba serikali kulipatia ufumbuzi tatizo la kupanda bei za bidhaa ili kuwaondoshea mzigo wananchi wa kipato cha chini.

Rai hiyo imetolewa jana na katika mkutano mkuu maalum wa wanachama wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini (kichama) uliohudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Hemed Suleiman Abdulla kilichofanyika katika ofisi za CCM Amani mkoa .

Waliesema hali ya sasa kwa bidhaa hasa za chakula hairidhishi jambo ambalo limepelekea kuwaumiza wananchi wakitolea mfano kupanda bei kwa bidha ya mkate na mafuta ya kupikia.

Akitolea ufafanuzi juu ya hoja hizo, Hemed alisema kuwa serikali imeshatoa maelekezo kwa wizara inayohusika na biashara kupanga namna bora ya bei za bidhaa ili zisiwaumize wananchi kwa ujumla.

Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  alisema serikali haitomvumilia mfanyabishara yoyote atakayekwenda kinyume na bei elekezi zinazotolewa na serikali na kuwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wafanyabiashara wanaokwenda kinyume na maelekezo ya serikali.

Akigusia suala la uongozi ndani ya chama, Hemed aliseam CCM ina taratibu zake za kikatiba za kuwapata viongozi hivyo aliwataka wanachama kuwa wavumilivu na kusubiri muda wa uchaguzi wa ndani ya chama na kuacha tabia ya kupanga safu.

Kuhusu tatizo la matumizi ya dawa ya kulevya, Hemed aliwaomba viongozi hao kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali kuu katika kupambana na kadhia hiyo ili kujenga taifa bora.

Alifafanua kuwa, Serikali itachukua hatua kali ikiwemo kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria kwa lengo la kuwadhibiti waltu wanaojihisisha na biashara hiyo haramu inayoharibu jamii ya wazanzibari.