NA HAFSA GOLO
VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kaskazini “B” Unguja, wamesema wanaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ilani, ahadi na utatuzi wa kero za wananchi walizoahidi viongozi wa majimbo yote mkoani humo, ili kuona utekelezaji wake unaleta ufanisi wa maendeleo.
Katibu wa CCM Mkoa huo, Mula Othman, alieleza hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mahonda ambapo alisema lengo ni kuona hatua zilizofikiwa na viongozi hao pamoja na changamoto zilizopo katika utekelezaji wao wa majukumu, ili viongozi hao waweze kutafuta mbinu mbadala zitakazoleta mafanikio.
Mula alisema Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo itahakikisha kinatimiza azma na malengo ya wananchi hasa katika suala zima la maendeleo majimboni.
“CCM ina sera na ilani nzuri zenye kutekelezeka jambo la msingi na lakuzingatiwa na viongozi ni uwajibikaji na ubunifu wenye kuleta mabadiliko ya kuichumi na kijamii”,alisema.
Aidha alisema moja ya mikakati ya viongozi wa mkoa huo ni kuona umoja na mshikamano kwa viongozi wa majimbo unaendelea kuimarika sambamba na kubadilishana uzoefu katika suala zima la kiutendaji.
Alifahamisha kwamba nguvu za pamoja zitasaidia kufikia malengo ya chama hicho pamoja na mipango ya serikali hasa kuwaletea mabadiliko ya maendeleo wananchi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Licha ya mipango hiyo Mula, alisema atahakikisha vijana wa CCM na wengine kwa jumla wanajengewa mazingira bora ambayo yatasaidia kuhamasisha uwajibikaji katika shughuli za maendeleo zinazofanywa na viongozi wa majimbo mkoani humo.
Alisema anaamini iwapo vijana watakuwa na kipaumbele cha kujitolea katika ujenzi wa miradi ya maendeleo majimboni itasaidia kuleta matokeo chanya ya ustawi wa maendeleo katika jamii zilizowazunguka.
Alifahamisha kwamba mpango huo utakuwa sambamba na uelimishaji wa umuhimu wa kutii sheria bila ya shuruti sambamba na maadili.
“Tutapowajenga vijana wetu katika misingi imara itasaidia kuimarika kwa uzalendo na kuheshimu mambo ya historian na tamaduni zao”,alisema.