Linahusisha visiwa vya Changuu, Bawe

Wasafirishaji watalii wasema Corona imetibua biashara hiyo

NA TATU MAKAME

CHABAMCA ni eneo maarufu visiwani Zanzibar liliopo maeneo ya Bandari ya Malindi.Eneo hilo ni hifadhi ya visiwa vya Changuu na Bawe ambalo limo katika hifadhi maalum hasa kwa shughuli za utalii.

Hifadhi hiyo imeanzishwa mwaka 2014 kupitia sheria namba 7 ya uvuvi ya mwaka2010 (Fisheries Act No 7 of 2010).Eneo hilo lina ukubwa wa kilomita za mraba zipatazo 118.2 na urefu wa kilomita 10 na lina visiwa vyenye urefu wa kilomita 6.

Awali katika miaka 1964 eneo hilo lilikuwa likitumika kwa shughuli za uvuvi ambalo pia liliwahi kutumika kama kambi ya Jeshi hadi mwaka 1978.

Hata hivyo mnamo mwaka 1978 mpaka 1992 eneo hilo lilikuwa ni sehemu ya kambi ya Dago kwa wavuvi (Fishing Camp) ambapo baadae imekuwa ni sehemu ya hifadhi ya mazingira hadi sasa.

Pamoja na mambo mengine, lakini eneo hilo limejaaliwa kuwa na raslimali nyingi za kiuchumi ikiwa ni pamoja na vivutio vya utalii ikijumuisha Fungu la nakupenda (Fungu pange).

Kwa miaka ya hivi karibuni eneo hilo limekuwa ni mashuhuri kwa biasha ya utalii ambapo kampuni za watalii hupeleka watalii visiwa vya Changuu na Bawe pamoja na fungu la nakupenda na hivyo kwa kiasi kikubwa kuingizia mapato serikali.

Katika makala haya tunazungumzia namna ya eneo hili la hifadhi ya Chabamca lilivyoathirika na janga la corona kwa kukosa kupeleka watalii hasa katika wimbi la kwanza la corona.

Aidha baada ya kujitokeza kwa ugonjwa wa Covid 19 mwaka 2019 duniani kote biashara hiyo ilipungua kwa asilimia kubwa katika eneo hilo.

Mwandishi wa Makala haya alifanya mahojiano na kampuni zinazosafirisha watalii ili kujua hasara walizopata baada ya kujitokeza ugonjwa huo visiwani Zanzibar na duniani kwa ujumla.

Monica Mosele ni mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya kusafirisha watalii ya ‘Nakupenda LTD’ kutoka Fungu pange na visiwa vya Chaguu na Bawe.

Mtembezaji huyo watalii alisema kujitokeza kwa ugonjwa wa Uviko 19 athari kubwa imejitokeza ikiwa ni pamoja na kukosa wateja wa uhakika wa kila siku.

Alisema kabla ya ugonjwa huo kuingia alikuwa akisafirisha wageni kutoka nchi mbalimbali duniani ambao walikuwa wakitembelea maeneo ya visiwa hivyo vilivyo katika kisiwa cha Unguja.

Alifahamisha kuwa mara ya kuripotiwa ugonjwa huo wageni wanaotembelea visiwani wamepunguwa kwa asilimia kubwa na kusababisha visiwa hivyo kupata idadi ndodo ya wageni wanaotembelea maeneo hayo.

Alisema kwa siku alikuwa akisafirisha wageni 40 hadi 50 na wakati mwengine huzidi idadi hiyo kabla ya ugonjwa wa uviko 19.

Monica ambae ni raia wa Italia yupo Zanzibar kwa zaidi ya miaka 14 sasa alisema kwa sasa husafirisha wageni kati ya watatu na watano kwa siku na mara nyengine kukosa kabisa.

“Tangu kuja kwa ugonjwa wa uviko19 hali ya utalii kwenye biashara hii haijarejea vizuri kwani zipo siku ambazo tunakosa hata wageni”, alisema.

Alisema hali hiyo imewakosesha haki zao za msingi na za binaadamu kutokana na wageni wengi kushindwa kutembelea eneo hilo na kukosa huduma nyengine za msingi.

“Ukipata mgeni kwa siku ujue unakula na kubakisha lakini kinyume na hivyo utakosa huduma siku inayofuata”, alisema.

“Ili tuendeshe maisha yetu lazima tusafirishe wageni na kupata chochote lakini kujitokeza kwa ugonjwa huu kumeleta athari kubwa kwetu wasafirishaji watalii”, alisema.

Sambamba na hayo alisema kujitokeza kwa ugonjwa huo wageni kutoka nchi za Italia wamepungua ambao ndio wanaotembelea kwa wingi sehemu za visiwa.

Nae Saidi Masoud Ali alisema kujitokeza kwa ugonjwa huo mapato yatokanayo na kusafirisha wageni kutoka bandari ya Malindi kwenda fungu pange na visiwa vya Changuu na Bawe yameshuka.

“Kawaida mgeni mmoja tunamsafirisha kwa bei ya shilingi 40,000 pamoja na chakula na tulikuwa tunapata wageni zaidi ya 50 kwa siku lakini hali ni ngumu kwa sasa”, alisema.

Alisema licha ya kuendelea na shuhuli zao lakini kushuka kwa wageni wanaotaka kwenda maeneo ya visiwani kunawakosesha matumaini ya kuendelea na kazi hiyo.

“Ndugu mwandishi wewe shahidi kabla ya ugonjwa huu, boti zote zilikuwa na wateja lakini angalia vyombo vilivyolala bila ya kuwa na wageni”, alisema.

Alisema ugonjwa huo umesababisha wafanyabiashara hao washindwe kuendelea vyema na majukumu yao ya kusafirisha wageni kutokana na biashara hiyo kupungua wateja.

Sambamba na hayo alisema wasafirishaji wageni wengi wao wameshindwa kuendesha familia zao kutokana na kukosa uhakika wa kupata wateja.

Nae Juma Mwinyi Said kutoka kampuni ya Safari, alisema kujitokeza kwa ugonjwa huo hapa Zanzibar biashara ya kutembeza watalii kwenye visiwa imeshuka kutokana na wageni wengi wanaoingia Zanzibar kuwa hawaoni umuhimu wa kutembelea visiwa.

“Kipindi hiki wapo wageni lakini sio wale wenye mwamko wa kutembelea visiwa kwani sisi wageni wetu wa kutembelea maeneo hayo walikuwa ni wageni kutoka Italia ambao kwa sasa bado hawajaznaza kuja hapa Zanzibar”, alisema.

Nae Khalmaf Masoud Maohamed ambae anafanya kazi ya kusafirisha watalii kutoka Bandari ya Malindi kwenda Fungu la Nakupenda alisema kujitokeza kwa ugonjwa huo wateja wao wamepungua kwa asilimia kubwa ukilinganisha na kipindi cha kabla ya ugonjwa huo hapa Zanzibar.

“Mara nyengine tunakuja hapa tukiona hatujapata wageni wanaokwenda funguni tunakwenda kutafuta harakati nyengine ili tupate riziki”, alisema.

Ali Juma Saada ambae anafanya kazi ya kusafirisha watalii kwenda Fungu la nakupenda alisema kujitokeza kwa ugonjwa wa uviko 19 wavuvi wengi wameendelea kufanya uharibifu wa mazingira sehemu za kutembeza watalii.

Alisema wavuvi hao hufika eneo la Fungu pange na kuchota mchanga hasa maeneo ya mafungu hali inayosababisha kuharibu maeneo hayo.

“Licha ya kukosa wageni pia tumeathirika kutokana na ndugu zetu wavuvi kufika maeneo hayo kufanya uharibifu wa mafungu, jambo ambalo linaweza kuhariba haiba nzuri ya eneo hilo”, alisema.

Hata hivyo aliitaka serikali kuongeza ulinzi katika eneo hilo ili sehemu hiyo iendelee kutumika kwa harakati za utalii, sambamba na kuipatia mapato serikali.

Nae Mratibu wa Masuala ya Elimu na mazingira na hifadhi ya visiwa vya Bawe, Changuu, Khamis Khalfan Juma, aliiambia makala haya kuwa kisiwa hicho kina historia kubwa ya kutembelewa na wageni lakini kujitokeza kwa ugonjwa wa uviko19 wageni wanaokwenda kisiwa hicho wamepungua.

Alisema hali hiyo imesababishwa na mwenendo mzima wa hali ya kiuchumi wa dunia na si Zanzibar pekee kwa wakati huu.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdalla Hussein Kombo, alisema serikali itashirikiana na wananchi ili kulinda mazingira ya bahari hasa katika maeneo ya hifadhi ili raslimali ya bahari ilete manufaa kwa taifa.

Alisema umefika wakati kushirikishwa wavuvi na wananchi juu ya umuhimu wa hifadhi ya mazingira ya bahari ili kulinda raslimali hizo.

Hata hivyo alizitaka kamati za uvuvi na uhifadhi wa mazingira kupambana na watu wanaojihusisha na uchafuzi wa mazingira ya bahari na kwamba wao wasiwe kigezo cha kuharibu mazingira ikiwa ni pamoja na kuharibu vianzio vya utalii ikiwa ni pamoja na mchanga wa mafungu.

Alisema ili kufanikisha azma hiyo Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imejipanga kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi na wavuvi ambao ndio watakaofanikisha malengo ya uhifadhi wa bahari.

RASLIMALI ZILIZOMO KWENYE VISIWA

Kuwepo kwa visiwa vidogovidogo kama vile Changuu, Bawe, Chapwani na kipandiko (Snake) na miamba kama vile mwamba Murogo, Mwamba Pange, sehemu ya mwamba Nyange pamoja na mafungu ya mchanga (Sandbanks).

Kuwepo kwa viumbe vinavyopatikana kama Kasa, Pomboo, Chongowe, Papa usingizi, samaki, majongo ya bahari, Majani bahari na mikoko.

HATUA ZA KUCHUKUA KUILINDA CHABAMCA

Moja ya hatua za kuilinda visiwa ni kuacha uvunaji wa matumizi ya mitego au njia zisizo kubalika za uvuvi, mabadiliko ya tabia nchi.

Uchafuzi wa mazingira, utiaji nanga,mmong’onyoko wa fukwe, uchomaji wa mkaaa na uchotaji wa mchanga kwenye mafungu.