NA TATU MAKAME

WAZIRI wa Maji, Nishati na Mazingira Suleiman Masoud Makame ameahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa wajasiriamali wa mama lishe na baba lishe wanaoendesha harakati zao katika kijiji cha Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Waziri Masoud alisema hayo Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini B Unguja wakati wa uzinduzi wa kikundi cha umoja wa mama lishe na baba lishe.

Alieleza kuwa huduma ya maji ndio inayomuwezesha kiumbe kuishi hivyo aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la maji kwa kushirikiana na viongozi wa jimbo na mamlaka husika ili wajasiriamali hao wapate huduma hiyo ipasavyo.

“Kiumbe yoyote anayeishi anategemea maji bila ya maji huwezi kuishi hivyo lazima tutafute ufumbuzi wa suala hili kwa wajasiriamali hawa”, alisema.

Sambamba na hayo Waziri huyo aliahidi kufuatilia suala hilo ili wajasiriamali wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuepuka usumbufu wanaoupata wa kutafuta huduma hiyo masafa marefu.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Asha Abdallah Mussa aliahidi kuwasaidia wajasiriamali hao kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais. Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa kufuatilia fursa za mikopo ili kikundi hicho kiweze kupatiwa mikopo.

Alisema kilio cha ukosefu wa huduma ya maji kwa akinamama na baba lishe kijijini hapo ni cha muda mrefu hivyo alimtaka Waziri huyo kufanya haraka kufuatilia suala hilo kuondosha usumbufu kwa wajasiriamali hao na kutimiza azma ya serikali ya awamu ya nane ya kuwasogezea karibu huduma muhimu wananchi.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili kujikwamua na umaskini.

Akisoma risala mwanachama wa umoja huo Mariyam Juma alisema kuanzishwa kwa umoja huo wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kujikwamua kiuchumi na kuweza kufungua akaunti kupitia benki ya NMB na kuweza kukopeshana.

Katika hafla hiyo jumla ya shilingi 1,000,000 zilitolewa ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wajasiriamali hao ambapo Waziri huyo alichangia shilingi 500,000 huku Mwakilishi wa Jimbo hilo nae kutoa shilingi 500,000.