WASHINGTON, MAREKANI

WAKATI chanjo ya corona ikiendelea kutolewa katika Mataifa mbalimbali Duniani, chanjo ya Virusi vya UKIMWI (VVU) iliyokuwa inafanyiwa utafiti muda mrefu na Kampuni ya Moderna ya Marekani ilitarajiwa kuanza kufanyiwa majaribio kwa Binadamu.

Kampuni hiyo imetengeneza chanjo za aina mbili za UKIMWI ambazo zimefuzu katika hatua za awali za kimajaribio na hivyo kuanza kutumika kwa binadamu katika awamu ya tatu.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, chanjo hizo ni mRNA-1644 na mRNA-1644v2-Core ambazo zimeshachunguzwa na kufanyiwa majaribio ya awali na kuonekana salama kabla ya kujaribiwa kwa Binadamu kwa mara ya kwanza.

Chanjo hiyo itaanza kutolewa kwa Watu 56 wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 56 na majaribio yanatarajiwa kukamilika Mwaka 2023.

Hatua hii imekuja baada ya kampuni hiyo ambayo inatengeneza chanjo za aina mbili za Ukimwi, kufuzu hatua za awali za kimajaribio na hivyo kuanza kutumika kwa binadamu katika awamu ya tatu.

Hivi karibuni ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI inaonyesha kuwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi au VVU wako katika hatari zaidi ya kuugua ugonjwa wa Corona au COVID-19 na hata kufariki dunia lakini bado wananyimwa haki ya kupata chanjo dhidi ya Corona.

Umoja wa Mataifa ulitangaza mwaka 2019 kwamba, watu milioni 38 kote duniani wanaishi na virusi hatari vya HIV, huku ugonjwa wa Ukimwi unaosababishwa na virusi hivyo ukiua watu 770,000 mwaka juzi 2018.