NA ABUBAKARI AKIDA, MOHA
MADEREVA wa bodaboda Visiwani Zanzibar wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na vifo vilivyoshamiri chanzo ikiwa kutofuatwa kwa sheria za usalama barabarani.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo alieleza hayo jana wakati wa kikao na madereva bodaboda wa Mkoa wa Mjini Magaharibi ambacho pia kilihudhuriwa na uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Serikali yenu sikivu chini ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi iko katika mchakato ili mruhusiwe kutoa huduma za usafiri katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, sasa nawaomba muanze kujifunza na kufuata sheria za usalama barabarani ili tunayoona yanayotokea kule bara yasitokee huku”, alisema.
Alisema kuna mambo kadhaa wameshaanza kuhusishwa nayo waendesha bodaboda kabla hawajaruhusiwa hivyo lazima wajiepushe ili lengo la serikali ni kuwatengenezea mazingira mazuri ya ajira liweze kukamilika.
Alisema baadhi ya mambo wanayohusishwa nayo waendesha bodaboda ni pamoja na ushiriki katika uhalifu ikiwemo vitendo vya uporaji, kukata watu mapanga ambapo mambo hayo sio mazuri na jeshi la polisi liko macho na halitosita kuwachukulia hatua.
Akizungumzia takwimu za ajali za bodaboda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji, alisema ajali na vifo vinavyotokana na bodaboda vimepungua kutokana na elimu inayotolewa kwa madereva hao.
“Mwaka huu tuna ajali 17, watu waliofariki mwaka jana ni watu 18 na mwaka huu tuna vifo 17 huku upungufu ukiwa ni mtu mmoja, lakini ajali zilizosababisha majeruhi kwa mwaka jana ni ajali 19 na mwaka huu ni ajali 6 kwa hiyo kuna upungufu wa ajali 15, watu waliojeruhiwa mwaka jana watu 37 na mwaka huu ni watu 6 kwahiyo tunaona kuna kushuka kwa ajali na athari zake” alisema RPC Awadh.
Wakizungumza kwa nyakati mbalimbali katika kikao hicho bodaboda hao waliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nia ya kuandaa utaratibu ili waweze kuruhusiwa kufanya kazi zao huku wakiahidi kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani.