NA TATU MAKAME
WIZARA ya Afya, Ustatawi wa Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar imepokea msaada wa dawa za aina mbalimbali kutoka serikali ya watu wa China.
Akipokea msaada huo huko hospitali ya Mnazi Mmoja, waziri wa wizara hiyo Nassor Ahmed Mazrui alisema dawa hizo zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 120.
Alisema serikali ya China iko mstari wa mbele katika kusaidia Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa huduma za matibabu na dawa.
“Hii ni mara ya pili kupokea msaada kama huu hivi karibuni tulipokea msaada wa dawa 165 katika hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba na sasa tumepokea kiwango kama hicho kutoka kwa ndugu zetu wa China”, alisema.
Hata hivyo aliishukuru serikali ya China kwa ushirikiano wao wa kutoa msaada wa huduma mbalimbali za matibabu ya afya ikiwemo kutoa madaktari na dawa za kutibu wagonjwa.
“Hata Ijumaa tulisaini mkataba wa ujenzi wa nyumba za wafanyakazi Mkoani Pemba kwa kweli tunatoa shukurani za dhati kwa ndugu zetu hawa”, alisema.
Balozi wa China nchini Tanzania, Zhang Zhisheng alisema wametoa msaada huo ikiwa ni kuendeleza mashirikiano na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kusaidia huduma za afya.
Alisema kwa muda mrefu China na Tanzania ikiwemo Zanzibar imekuwa na uhusiano wa karibu hivyo kutoa dawa hizo ni kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na China.
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili nje ya hospitali hiyo wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Unguja waliishukuru serikali ya China kwa juhudi inayochukua ya kuongeza dawa na kupunguza changamoto inayowakabili wagonjwa ya kukosa dawa kwa wakati.
Wananchi hao walisema kuletwa kwa dawa hizo kutaondosha kero wanayoipata wananchi ya kufuata huduma za dawa na matibabu katika vituo binafsi na kuongeza Imani kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kupata huduma bora za matibabu.