NA AMEIR KHALID
CHUMBE Island Coral Park kwa kushirikiana na Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi (DCMA), wamefanya mashindano ya kuimba kwa wanamuziki wa Zanzibar.
Mashindano hayo walitakiwa kuwashirikisha wasanii wa Zanzibar, kwa kutunga na kuimba nyimbo mbali mbali.
Akizungumza na gazeti hili msaidizi meneja katika kitengo cha uhifadhi na utoaji elimu Chumbe Island Coral Park Enock Bartholomelo, ambao ndio wadhamini wa mashindano hayo, alisema mashindano hayo yalikuwa na lengo la kutangaza utalii wa mazingira wa Zanzibar.
Alisema katika mashindano hayo walitoa mada maalum ambazo msanii alitakiwa kutungia nyimbo.Alizitaja mada hizo ni upekee wa Zanzibar, uzuri wake, rasilimali zilizopo na kitu gani kinaweza kumvutia mgeni au mtalii kutembelea Zanzibar.
Alisema kila msanii alikuwa huru katika mashindano hayo kushiriki na njia ya kushiriki ni kutumia ‘Whatsapp’, kwa kurikodi sauti na kutuma katika namba maalum waliopewa.
‘’Sauti hizo zilipelekwa kwa majaji na baadayE kufanywa mchujo na majaji hao, na kupatikana washindi watatu ambao watatangazwa muda wowote na kupatiwa zawadi, ya shilingi 100,000 mshindi wa kwanza, wa pili 80,000 na 60,000 kwa watatu, pamoja na kurikodi nyimbo katika studio bure’’alisema.