NA KHAMISUU ABDALLAH

VIJANA wa kiume wameshauriwa kutumia fursa zilizokuwepo katika vyuo mbalimbali vilivyokuwepo nchini ili kuweza kujipatia ujuzi na kuweza kujiajiri wenyewe.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Ushoni Mafunzo ACP Mwanahija Ismail Mtuli, wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Kilimani Mjini Unguja.

Alisema, ikiwa vijana wataweza kutumia fursa hiyo basi kwa kiasi kikubwa wataweza kujiajiri na kuondokana na tabia ya kukaa katika vigenge ambavyo vinawaharibia maisha yao.

Aidha alisema Chuo cha Mafunzo kina chuo cha ushoni na kutoa fursa kwa watu wa nje kuweza kujifunza, lakini idadi ya wanafunzi wengi wao ni wanawake ukilinganisha na watoto wa kiume.

“Hapa chuoni kwetu wanafunzi wote kutoka nje ni 48, lakini vijana wa kiume ni sita tu hii inaonesha wazi kuwa vijana wa kiume kuona kazi hii inafanywa na wanawake pekee jambo ambalo sio la kweli,” alisema.

Mkuu Mwanahija, alibainisha kuwa kazi ya ushoni ni kama kazi nyengine ambazo zinawawezesha watu kupata kipato na kuweza kumudu maisha yao ya kila siku.

Hivyo, aliwasisitiza ni wakati kwao sasa kuamka na kuiona kazi ya kushona ni kazi kama kazi nyengine ambayo inaweza kuwapatia kipato na kuweza kujiajiri wenyewe.

Aliwasisitiza wazazi na walezi kujitahidi kuwahimiza watoto wao pale wanapokataa kusoma au wanaomaliza masomo kutowaacha kukaa majumbani na kuanza kuzurura ovyo na badala yake kuwapeleka kwenye vituo vya ufundi, ili waweze kujipatia ujuzi.

“Umefika wakati sasa kwa sisi wazee kuamka kwani mtoto yeye mwenyewe sio rahisi, wazazi wanawake ambao ndio walezi wakuu kwa watoto wetu tuwajengee misingi mizuri watoto wetu katika maisha yao ya baadae,” alisisitiza.