NA ATATU MAKAME

OMAR Juma Hassa (24) mkaazi wa Amani wilaya ya Mjini, amepandishwa katika kizimba cha mahakama ya mkoa Mwera, kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya.

Mwendesha Mashitaka, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Safia Serembe, aliwasilisha jadala la mshitakiwa huyo mbele ya Hakimu Saidi Hemed Khalfan.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya kete 13 za unga aina ya heroini wenye uzito wa gramu 0.1517.

Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na dawa hizo Juni 30, 2019 huko Paje wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja majira ya saa 12:30 jioni.

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 15 (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2009, ambacho kilifanyiwa marekebisho na kifungu cha 11 (a) cha sheria namba 12 ya mwaka 2011.

Hata hivyo mshitakiwa huyo anatarajiwa kurejeshwa mahakamani Agosti 23 mwaka huu kesi yake itakapoanzwa kusikilizwa.