NA HAJI NASSOR, PEMBA

MKUU wa Wilaya ya Chake chake, Abdalla Rashid Ali, amesema kazi inayofanywa na Idara ya Msaada wa Kisheria, inafaa kuungwa mkono na jamii, kwani suala la kupata haki na kujua wajibu lipo kikatiba.

Mkuu huyo wa wilaya, aliyasema hayo mjini Chake chake, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu, ya uandishi wa ripoti na madili yanayoendeshwa na Idara ya msaada wa Kisheria Zanzibar kwa kushirikiana na UNDP.

Alisema jamii ya Zanzibar, inahitaji kupata uwelewa juu ya haki zao mbali mbali, hivyo kazi inayofanywa na Idara hiyo kwa kuwatumia watoa msaada wa kisheria, lazima iungwe mkono na kila mmoja.

Mkuu huyo wa Wilaya, alieleza kuwa, Idara hiyo, ambayo imeanzishwa chini ya sheria nambari 13 ya mwaka 2018, kwa sasa imekuwa mdau mkuu wa haki za binadamu, katika kuwatambulisha watu haki zao.

“Pamoja na kazi zenu nyingi mnazozifanya, lakini Idara hii imekuwa mkombozi kwa jamii ya Zanzibar, kwa kuwaelimisha haki na wajibu wao, jambo hapo awali lilikuwa likiwawiya vigumu,’’alieleza.

Kuhusu mafunzo ya uandishi bora wa ripoti na maadili kwa watoa huduma wa msaada wa kisheria waliopo Pemba, Mkuu huyo wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, alisema ni vyema kwa washiriki wakawa makini ili kujifunza zaidi.

Alisema, kama sio Idara hiyo ya Msaada wa kisheria kuwapatia mafunzo hayo, wengelazimika kwenda masafa maraefu kuyatafuta, hivyo ni lazima wawe makini wanaposomeshwa.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alisema wanaendelea na mradi huo, ili kuhakikisha watoa msaada wa kisheria wanafanya kazi zao kwa ufanisi.

“Lazima niipongeze serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha Idara hii, maana sasa imekuwa ni kimbilio hasa kwa wanyonge, ambao wanaelekea kukata tamaa kupatikana kwa haki zao,’’alifafanua.

Kuhusu mafunzo hayo ya uandishi bora wa ripoti na maadili, waliona ipo kasoro kwenye ripoti zao za robo, nusu na mwaka na kuwemo kwa maelezo mengi yanayokosa ushahidi wa takwimu.

Mapema Afisa Sheria kutoka Idara hiyo Zanzibar, Ali Haji alisema sasa anaamini kuwa, baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, uandishi utakuwa wenye kueleweka na kufahamika.

Akiwasilisha namna ya kuandika habari hizo, Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Harusi Miraji Mpatani, alisema lazima ripoti zitumie lugha laini na yenye kufahamika.

Alisema, jengine ni kuhakikisha wanatumia takwimu, mifano halisi na hai, ufafanuzi wa kina, ili kumsaidia mwengine ambae hakuwepo kwenye matukio.

Baadhi ya washiriki akiwemo Riziki Hahamd Ali kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake alisema, mafunzo hayo watayatumia vyema.

Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Katiba, sheria, Utumishi na Utawala bora chini ya Idara ya Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana na Shirika la ‘UNDP’ inaendeleza mradi wa Uwezeshaji Kisheria na Upatikanaji Haki wa miaka mitatu, ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Mradi huo ambao unajishughulisha na upatikana wa haki pia unazisimamia Idara za Mahakama, wizara husika ya katiba na sheria, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya mwanasheria Mkuu.

Idara ya Msaada wa Kisheria ambayo imeanzishwa chini ya sherai nambari 13 ya mwaka 2018 na kwa mujibu wa ripoti yake ya mwaka 2019/2020 imeeleza kuwa, watoa huduma wamewafikia wananchi 122,149 wa Unguja na Pemba.

Kati ya hao, wanawake 63,834, wa wanaume 54,334 ambapo watoto wa kiume walikuwa 3,029 wakike walifikiwa 952 ambapo wote walipata msaada wa aina mbali mbali wa sheria bila ya malipo.