NA KHAMISUU ABDALLAH

KITENDO cha dereva kuendesha gari akiwa amelewa, kimemsababisha kutozwa faini ya shilingi 150,000 katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe.

Mshitakiwa huyo ni Mohammed Ameir Ibrahim (27) mkaazi wa Dole Unguja, alitozwa faini hiyo na Hakimu Omar Said Khamis, baadaa ya kukubali kosa lake aliloshitakiwa mahakamani hapo la kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa.

Akitoa hukumu kwa mshitakiwa huyo, Hakimu Omar alisema, mahakama inamuona kwamba mshitakiwa huyo ni mkosa kisheria na kumtaka kulipa faini ya shilingi 150,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki tatu.

Adhabu hiyo dhidi yake, imetolewa chini ya kifungu cha 23 (1) (b) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kama alivyotakiwa na mahakama.

Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Suleiman Yussuf, alidai kuwa, mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa, kinyume na kifungu cha 123 (1) (b) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa, Juni 24 mwaka huu majira ya saa 2:00 za usiku huko Masingini wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, akiwa dereva wa gari yenye nambari za usajili Z 414 KF P/V akitokea Mtofaani kuelekea Welezo, alipatikana akiwa anaendesha gari hiyo barabarani akiwa amelewa.

Wakili Suleiman alidai kuwa, mshitakiwa huyo alishindwa kuiongoza vyema gari yake na baada ya kupimwa, alipatikana akiwa na kiwango cha ulevi 81.9 mg/100 ml kitendo ambacho ni kosa kisheria.