NA HAFSA GOLO

KATIKA taifa lolote duniani jambo la kwanza ni kuona uchumi wan chi unakuwa imara jambo ambalo hata Zanzibar nayo inataka kuwa hivo.

Kutokana na hilo, ndio maana nchi mbali mbali zinahakikisha inaimarisha vianzio vyake vya mapato kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi.

Hivyo basi serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya Nane ina dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili kujenga uchumi imara kwa Taifa.

Hatua hiyo ya serikali  bila shaka ni jambo muhimu hasa katika nchi za visiwa ikiwemo Zanzibar ambayo imezungukwa na bahari.

Aidha mikakati na mipango hiyo ya serikali ni ya msingi kwani yamedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi sambamba na wananchi waweze kupata fursa mbadala za ajira.

Itakumbukwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  mnamo Juni 12, 2021 huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde nje kidogo ya Jiji la Zanzibar wakati akifungua Kongamano la siku moja lililobeba  mada “Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi  na Uhifadhi wa Mazingira Zanzibar”.

Kongomano hilo malengo ni kuona Zanzibar inaweza kutumia rasilimali bahari katika kuimarisha masuala ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii.

Kwa mujibu wa maelekezo yake  Dk. Mwinyi alifahamisha bado kuna fursa, faida na vipaumbele vya uwekezaji zaidi chini ya Uchumi wa Buluu kama vile katika sekta za uvuvi mdogo mdogo, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji samaki na mazao ya bahari.

Kwa mukhtadha huo watendaji wenye dhamana katika maeneo yao ya kazi wana wajibu wa kuandaa mipango kazi ya kuishajihisha jamii ili iweze kutumia rasilimali hizo vyema kwa dhamira ya maendeleo.