NA ABOUD MAHMOUD

WANANCHI wanaoishi katika maeneo ya Mtoni Kidatu na  Mtopepo, wameiomba Serikali kuwasaidia kuwajengea mtaro ambao utaondosha kero inayowakabili.

Hayo waliyasema wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, alipofanya ziara ya kutembelea maeneo hayo.

Wananachi hao, walisema wamekua na tatizo na miaka mingi hali inayoyawafanya kila ikinyesha mvua kusababisha kupoteza vitu mbali mbali ikiwemo kufariki kwa watoto.

Walisema kwamba mara baada ya kujengwa kwa barabara ya pili inayoanzia Amaan na kumalizikia Mtoni mtaro huo umeziba na kufanya maji yanayopita hapo kuziba na kuingia kwenye nyumba za wananchi.

“Tunaiomba Serikali yetu kutuisaidia kujenga huu mtaro, sisi wananchi tupo katika hali mbaya ikinyesha mvua tu basi roho zetu zinakua juu inatulazimu tuhame sisi na vitu vyetu,”alisema Hafsa Msabah Hassan.

Nae Mwatima Haji Ali alisema ,kitendo kilichotokea baada ya mtoto kufariki kwa kuchukuliwa na maji, wakati wakiwa wanapanda kwenye bati, ili kujinusu na na maji yalioingia ndani kimewaathiri wananchi wote katika maeneo hayo.

“Hapa tunaishi kwasababu hatuna sehemu nyengine ya kwenda lakini tukiona wingu tu roho zetu zinafujika maana tunaishi kwa wasiwasi, na kitendo cha kufa yule mtoto kimetuathiri sana mana hata wenyewe wamehama hapa mtaani baada ya kutokea tukio lile,”alisema Mwatima.

Aidha wananchi hao walisema mbali na tatizo hilo la mtaro lakini pia wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa muda miaka kumi sasa, hali inayowafanya kutumia maji yasio salama yanayotoka kwenye mto.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum alisema atakutana na Waziri husika kujua jinsi ya ujenzi wa mitaro hiyo.

Alisema kutokana na ziara hiyo kuandaliwa na Mbunge atajitahidi kuchukua jitihada za kwenda na Waziri anaehusika na maswala hiyo ili kusikiliza kilicho cha wananchi hao.

Aidha, Dk. Mkuya, aliwaomba wananchi wanaoishi katika maeneo hayo  kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

“Hili tutalichukua na tunaenda kukaa na wenzetu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na kufatana na Waziri ili kuja kusikiliza hili tatizo linalokukabilini,”alisema.