NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amefanya uteuzi wa wakurugenzi na mthamini mkuu wa serikali katika wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, ilieleza kuwa uteuzi huo umeanza Agosti 26, mwaka huu.

Katika taarifa hiyo, Mhandisi Zena alieleza kuwa Muchi Juma Ameir ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa Idara ya Mipango Miji na vijiji na Juma Ameir Mgeni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Upimaji na Ramani.

Aidha Khamisuu Hamid Mohamed ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi na Tahir Mussa Omar ameteuliwa kuwa mthamini mkuu wa serikali.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi jana alikutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Jamhuri ya Msumbiji nchini Tanzania, Balozi Ricardo Amrosio Mtumbuida aliyefika kujitambulisha, ikulu Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Dk. Mwinyi alipongeza ushirikiano uliopo kati ya nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hasa katika ulinzi wa amani.

Kwa upande wake, Balozi Ricardo Amrosio alitoa pongezi Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020 na kushika wadhifa wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislam ya Pakistan nchini Tanzania, Balozi Muhammad Saleem na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kimaendeleo na uhusiano wa kibiashara.

Dk. Mwinyi alisema kuna umuhimu wa Pakistan kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa Zanzibar katika sekta binafsi kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (Zanzibar Chamber of Commerce) kwa kutembeleana kuimarisha mahusiano na fursa za kibiashara.

Kwa upande wake, Balozi Muhammad Saleem alisema Zanzibar inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na Pakistan kutokana na ushirikiano uliopo wa kibalozi kupitia sekta za elimu, Uchumi wa Buluu, biashara na fursa za masomo.