NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, jana alikutana na kufanya mazungumzo na  kamisaa mkuu wa  Sensa ya Watu na Makazi Tanzania, Anne Semamba  Makinda, hafla iliyofanyika ikulu mjini Zanzibar.

Makinda ambaye ni spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimuarifu Dk. Mwinyi kuwa maandalizi ya sensa itakayofanyika mwakani  mwezi Agosti mwaka 2022 yanaendelea vizuri.

“Kwa upande wa Zanzibar maeneo ya Sensa yametengwa kwa asilimia 40 mpaka sasa na zoezi linaendelea vizuri, tunatarajia kumaliza ndani ya muda”, alisema Makinda.

Aidha, Makinda aliyeongozana na kamisaa wa Sensa  Zanzibar, Balozi Mohamed Hamza, alisema sensa ya mwaka 2022 itatumia mfumo wa uingizwaji wa taarifa kwa njia za kidigitali ambapo kwa mara ya kwanza itajumuisha pia idadi ya majengo nchi nzima.

Kwa upande wake, Dk. Mwinyi alimuhakikishia Kamisaa Makinda kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kutoa ushirikiano wote utakaohitajika katika kuratibu zoezi zima la sensa ya mwaka 2022.

Dk. Mwinyi alisema, sensa ni zoezi muhimu kwa serikali na wadau mbalimbali, kwani takwimu zitakazokusanywa zinatumika katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Katika tukio jingine, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa wizara ya Katiba na Sheria uliiongozwa na waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi aliyefika ikulu jana mjini  Zanzibar.

Prof. Kabudi alimueleza Dk. Mwinyi kwamba madhumuni ya ziara yake ni azma ya wizara ya Sheria na Katiba katika kujifunza kutoka Zanzibar juu ya namna ya uandikaji wa sheria na matumizi ya lugha ya kiswahili kwenye huduma za kisheria