NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha viongozi aliowateuwa hivi karibuni katika taasisi za serikali.

Walioapishwa ni Dk. Omar Dadi Shajak anaekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Khadija Khamis Rajab aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya kazi na uwezeshaji katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Aidha Dk. Mwinyi pia amemuapisha Dk. Habiba Hassan Omar kuwa Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya Uchumi na Uwekezaji katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Dk. Fatma Mrisho kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto.

Dk. Mrisho aliyewahi kuwa mkurugenzi mkuu wa tume ya UKIMWi Tanzania (TACAID), anachukua nafasi ya Dk. Shajak ambapo pia Dk. Mwinyi alimuapisha Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khamis Kona Khamis ambae aliteuliwa Julai 16 mwaka huu.

Wakizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kuapishwa, viongozi hao walimshukuru Dk. Mwinyi kwa kuwaamini na kuahidi kufanya kazi kwa uadilifu na umahiri ili kufanikisha malengo ya taasisi wanazoziongoza.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khamis Kona Khamis alisema atashirikiana na watendaji wengine wa tume hiyo ili kufanikisha majukumu ya tume yao.

“Nitahakikisha naimarisha mashirikiano baina ya watendaji wa tume hiyo wakiwemo wajumbe wake na wadau wa uchaguzi kusimamia na kutekeleza majukumu yaliyoainishwa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya kuanzishwa kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar,” alieleza Kona.

Kwa upande wake Khadija Khamis Rajab, alisema matarajio yake ni kufanya kazi kwa kufuata, sheria, miongozo na kanuni zilizowekwa kwa uadilifu ili kutimiza malengo yaliyopangwa.

Alibainisha kuwa ofisi anayoifanyia kazi kwa kiasi kikubwa ina sekta zinazogusa jamii hasa ya wajasiriamali na ajira, hivyo atahakikisha mafanikio yanapatikana ili kufikia malengo ya wajasiriamali wa Zanzibar.