NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza ushirikiano kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ili kkukusanya kodi ipasavyo.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Alphayo Japan Kidata akiwa na ujumbe walipofika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.

Katika maelezo yake , Dk. Mwinyi alisema kuwa kuna haja ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na  Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufanya kazi kwa pamoja na azma ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa mashirikiano ya pamoja kati ya taasisi hizo mbili kutaondosha changamoto zilizokuwepo hapo siku za nyuma ambapo ukusanyaji wa kodi kwa upande wa Zanzibar haukuwa ukifanyika vyema.

Alisema kufanya kazi kwa pamoja kati ya taasisi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa na kuondosha upotezaji wa kodi sambamba na kutokuwa kikwazo katika kupatikana kodi hiyo.

Aidha, Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa juhudi zake inazozichukua katika ukusanyaji wa kodi hapa nchini.

Alifahamisha kwamba hata kwa upande wa Zanzibar ufanisi umekuwa mkubwa lakini hata hivyo, haja ya kuimarisha ushirikiano ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa wataalamu watakaosaidia ukusanyaji wa kodi.

Alisisitiza kwamba ni vyema mafanikio yaliopatikana Tanzania Bara kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) yakafanywa pia, kwa upande wa Zanzibar ili Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), iweze kufanya kazi zake ipasavyo.

Nae Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Japan Kidata alimuhakikishia Dk. Mwinyi kwamba Taasisi yake imekuwa na mashirikiano na Bodi ya Mapato Zanzbar (ZRB) na inaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha ndoto za viongozi wakuu zinafikwia.

Alieleza kwamba (TRA), imeweka mikakati kabambe katika kuhakikisha uwezo na uweledi uliopo katika Taasisi hiyo kwa upande wa Tanzania Bara pia, unafanya kazi kwa upande wa Zanzibar ili kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.