NA KHAMIS MOHAMMED

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka wahasibu wanawake nchini Tanzania kuendelea kufanyakazi kwa ufanisi na bidii ili kuleta maendeleo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Hayo aliyaeleza alipokuwa akifungua kongamano la nne la uongozi la wanawake wahasibu Tanzania huko katika hoteli ya Verde jijini Zanzibar jana ambapo hotuba yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.

Dk. Mwinyi, alisema, serikali inatambua umuhimu wa fani ya uhasibu kwani imekua sehemu ya kuwezesha ukuaji wa uchumi hasa katika kuhakikisha mahesabu yanafanyika vizuri na mikakati ya maendeleo ikipata mafanikio.

Alisema, wanawake wahasibu Tanzania kama sehemu ya kusaidia na kushirikiana na jamii kwa kufahamu umuhimu wa kuwezesha fani ya uhasibu, imekua mfano mzuri wa kuwa na wahasibu wanawake wengi ambao wamekuwa chachu ya maendeleo nchini.

Dk. Mwinyi, alisema, anafurahishwa kuona viongozi wakubwa wa taasisi mbalimbali nchini ni wanawake na taasisi hizo zimekua zikifanya vizuri kiutendaji.

“Mifano ipo mingi juu ya hili, rais wa Tanzania sasa ni mwanamke, lakini, pia Katibu Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar ni mwanamama. Taasisi nyingi viongozi wao ni akinamama ambao tumewashuhudia wakifanya vizuri, ni jambo la kujivunia”.

Hivyo, aliwataka akinamama hao kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilrifu wawapo kazini na badala yake wafanyekazi kwa bidii, uadilifu, umakini kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu za kitaaluma zilizowekwa.

“Vitendo vya rushwa na ubadhirifu vina madhara makubwa kwa maisha ya mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa letu kwa ujumla, ni vyema kila wakati mkumbuke kuwa rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya taifa”, alisema, Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi, alisema, fani za uhasibu ikiwemo ukaguzi ni muhimu katika kuendesha uchumi wa viwanda, hivyo, umahiri wa wataalamu wanaozalishwa katika taasisi hiyo unatakiwa kuonekana katika kukabiliana na changamoto za usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma na mahitaji ya soko.