NAIROBI, KENYA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imesema imeanza kutekeleza mpango juu ya maji, afya na usafi (WASH), ili kuongeza uwezo wa nchi wanachama katika kukinga na kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kwenye maeneo yenye hatari ya kutokea magonjwa hayo.

Makao makuu ya EAC yalitoa taarifa mjini Arusha, Tanzania, yakisema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la uhamiaji la kimataifa (IOM).

Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata Euro milioni 1.5 kutoka serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kufadhili mpango huo, ambao unalenga watu na maeneo yenye hatari kubwa ya kuambukizwa katika nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda, na watu zaidi ya milioni moja watanufaika na mpango huo.

Naibu katibu mkuu wa EAC anayeshughulikia sekta za uzalishaji na jamii Christophe Bazivamo alisema, mpango huo ni kwa ajili ya kukuza ufahamu wa watu juu ya ulinzi wa afya na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na COVID-19.