YAMOUSSOUKRO, IVORY COAST

SHIRIKA la afya duniani WHO limesema kwamba kesi ya kwanza ya Ebola imetangazwa mjini Abidjan wenye zaidi ya idadi ya watu milioni nne,ambacho ni kisa cha kwanza baada ya kipindi cha miaka 25.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, maofisa wa WHO walisema kwamba haijabainika iwapo maambukizi hayo yana uhusiano na yale yaliyotokea mwaka huu kwenye nchi jirani ya Guinea.

Mgonjwa aliyepatikana Abidjan na ambaye sasa anapokea matibabu, ni mwanamke mwenye umri wa miaka 18 anayesemekana kuwasili mjini humo kwa basi akitokea Guinea.

Waziri wa afya wa Ivory Coast Pierre N Gou Demba,alisema kuwa mgonjwa huyo aligundulika kuwa na Ebola siku iliyofuata na mara moja akaanza kupatiwa matibabu.

WHO limesema kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini iwapo maambukizi hayo mapya yana uhusiano na yale ya awali ya Guinea.

Mkuu wa WHO tawi la Afrika Dkt Matshidiso Moeti alisema kuwa ni suala la kutia wasi wasi kuona kuwa mgonjwa huyo amepatikana kwenye mji wa Abidjan.