KINGA ni bora kuliko tiba. Hii ni kauli mbiu ya muda mrefu inayotumika kusisitiza umuhimu wa kuzuia madhara makubwa mapema katika nyanja mbali mbali hasa afya.

Kauli mbiu hii ina mantiki Sana linapokuja swala la kujikinga na madhara ya maradhi hasa Yale yenye kuepukika kwa kutumia kinga iwe ya ndani au nje ya mwili.

Wataalamu wa afya wamekuwa wakitusisitiza umuhimu wa kutumia nyenzo na mbiu tofauti kujikinga na maradhi, lengo ikiwa ni kuulinda mfumo wa ndani ya mwili wa kujikinga na maradhi.

Kwa mfano katika maradhi ya Covid 19 yaliyoenea ulimwenguni, mbali ya msisitizo wa watu kupokea chanjo ya kujikinga na maradhi hayo, bado msisitizo wa kutumia njia nyengine za kujikinga umeendelea kuwekwa.

Miongoni mwa njia inayotumika zaidi pamoja na zile za iujiweka katika hali ya usafi, matumizi ya barakoa (maski) hasa katika maeneo ya umma ni jambo linalosisitizwa.

Hii inatokana na ukweli kwamba kwa kutumia vifaa hivyo, kunapunguza uwezekano wa kuenea kwa virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwengine.

Tunapongeza mwitikio wa wananchi juu ya matumizi ya barakoa au maski Kama njia mojawapo ya kujikinga na maradhi haya lakini tunashauri haja ya kutolewa elimu ya matumizi sahihi na uhifadhi wake baaa ya matumizi.

tunasema hivyo baada ya kuona barakoa zilizotumika zikizagaa mitaani au karibu na maeneo ya hospitali au majengo ya umma yaliyoweka utaratibu wa kutoingia bila ya kuvaa barakoa.

Tunadhani kutupwa ovyo baada ya matumizi yake sio jambo jema kwani inaweza kuwa sababu ya kueneza maradhi haya na mengine pale barakoa yenye maambukizo itakapotumiwa na mtu mwengine hasa watoto wadogo.

Katika baadhi ya maeneo, watoto wadogo na hata watu wazima kuna taarifa kwamba wamekuwa wakitumia barakoa zilizotumika na wengine kuazimana ili waweze kuvuka mageti ya taasisi wanazoenda kupata huduma.

Jambo hilo ni hatari lakini bila shaka linatokea kutokana na uelewa mdogo juu ya matumizi ya silaha hiyo katika vita hii dhidi ya adui maradhi.

Hivyo tunaomba mamlaka zinazohusika na maswala ya afya kuendelea kusisitiza matumizi ya barakoa sanjari mamna bora ya uhifadhi baada ya matumizi ili kuepusha uchafuzi wa mazingira na kueneza maradhi ya corona na mengine yanashabihiana nayo.