KAMPALA, UGANDA

KIKOSI kazi cha Wilaya ya Budaka kinachoshughulikia Covid-19 kimevunjwa baada ya ripoti kuibuka kuwa baadhi ya familia zinafukua mabaki ya jamaa zao ili kuwapa haki ya kuwazika.

Ilielezwa kuwa familia kwa nyakati tofauti walilalamika kwa viongozi wao wa mitaa kwamba roho za jamaa zao waliokufa zinawasumbua usiku, wakidai kuzikwa kwa heshima kulingana na mila zao zilizowekwa.

Mkuu wa Wilaya Mkaazi (RDC) Tom Chesol, alithibitisha ripoti hizo akisema wenyeji wamekuwa wakifukua miili hiyo haswa usiku.

Chesol alisema jamaa wanadai marehemu wanalalamika juu ya joto linalotokana na mifuko ya polythene ambayo wamezikwa na timu ya mazishi ya Covid-19.

Alisema viongozi wataitisha mkutano wiki hii kutafuta njia za kushughulika na makamu huyo.

“Tunalaani kitendo hicho na tunatoa wito kwa wenyeviti wote wa baraza la mitaa kuwaonya wahusika kuwa wakikamatwa wataadhibiwa vikali,”alisema.

Mwenyekiti wa LCI katika mji wa Budaka Abdul Rashid, alisema mtoto wake wa kambo alihamasisha jamaa wengine kufukua mwili wa kaka yake, ambao ulizikwa wiki iliyopita baada ya marehemu kuripotiwa kumtokea.

“Marehemu aliripotiwa kumwambia kwamba alikufa kwa uchawi na sio Covid-19, kwa hivyo alihitaji mazishi yanayofaa,” alisema.

Jenifa Naloongo, katibu wa maswala ya wanawake katika Halmashauri ya Mji wa Budaka, alisema vitendo vya baadhi ya wenyeji vinadhoofisha juhudi za serikali kupambana na kuenea kwa ugonjwa huo.

“Hali hiyo inakuja wakati ambapo wilaya bado inajitahidi kuzuia kuenea kwa ugonjwa ambao hadi sasa umewaua watu sita katika eneo hilo,” alisema.