ZURICH, Uswisi
SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limempiga marufuku makamu wake wa zamani wa rais na rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Issa Hayatou kwa mwaka mmoja.
Shirikisho hilo lilimkuta raia huyo wa Cameroun mwenye umri wa miaka 74 na hatia ya kukiuka kifungu kinachohusiana na ‘wajibu wa uaminifu’ katika kanuni za maadili.
Uchunguzi wa Fifa ulilenga kuhusika kwa Hayatou katika mikataba iliyopigwa na Lagardere Sports juu ya “vyombo vya habari na haki za uuzaji za mashindano yaliyoandaliwa na Caf” wakati alipokuwa rais wa baraza linaloongoza la mpira wa miguu barani Afrika.
Mkataba huo wa miaka 12 ulisainiwa mnamo 2015 na ulianza kutumika mnamo 2017 na ulikuwa na thamani ya dola bilioni moja.
Kufuatia kusikilizwa kwa kina, kamati ya uamuzi ya FIFA iliamua kwamba, kulingana na habari zilizokusanya kwamba Hayatou aliingia ‘katika makubaliano ya kupinga ushindani na Lagardère Sport ambayo yalikuwa mabaya na yalisababisha uharibifu mkubwa kwa Caf.”
Uamuzi huo unamaanisha kwamba Hayatou amepigwa marufuku kushiriki katika aina yoyote ya shughuli zinazohusiana na mpira wa miguu katika kiwango cha kitaifa na kimataifa kwa mwaka mmoja na pia alitozwa faini ya zaidi ya dola 33,000.
Zuio hilo, ambalo linaanza kutekelezwa tarehe 3 Agosti, linamaanisha kuwa hawezi kushiriki katika Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Januari ambayo yanafanyika nchini mwake, Cameroun. (Goal).