LUSAKA, ZAMBIA
TUME ya taifa ya uchaguzi nchini Zambia imemtangaza Hakainde Hichilema kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita, akimbwaga rais wa sasa Edgar Lungu.
Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi ya Zambia Esau Chulu aliyatangaza matokeo rasmi asubuhi ya jana, baada ya kupatikana hesabu za majimbo yote isipokuwa moja tu.
Hesabu hizo zilionyesha kuwa Hakainde Hichilema wa chama cha United Party for National Development (UPND) amepata kura 2,810,777 akimpita rais wa sasa Edgar Lungu kutoka chama cha Patriotic Front (PF) aliyepata kura 1,814,201.
Wapiga kura milioni saba walikuwa wamejiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo yenye idadi jumla ya wakaazi karibu milioni 19.
Rais Lungu alisema uchaguzi huo haukuendeshwa katika mazingira huru na haki, na kutishia kukataa matokeo yake. Hii ilikuwa mara ya sita kwa Hakainde Hichilema kugombea wadhifa huo.