NA MADINA ISSA

JAJI Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, ameeleza kuwa masuala ya haki za binaadamu ni miongoni mwa mambo ya msingi katika nchi kwa kuwa yanagusia stahiki ambazo zinampaswa kila binaadamu kuzifaidi.

Jaji Makungu alisema hayo  wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa Wanasheria na Mawakili, yaliyoandaliwa  na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yanayofanyika katika hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Unguja.

Alisema kuwanyima watu haki zao ni sawa na kuukanusha ubinaadamu wao na hakuna haki zenye uzito ambazo binaadamu anapaswa kuwa nazo, zaidi ya haki za binaadamu.

Aidha alisema matumaini ya mkusanyiko huu pamoja na mambo mengine wataweza kutajadili namna ambavyo mawakili wanapaswa kuendesha kesi zenye maslahi kwa umma, haki za binaadamu, uhuru wa kujieleza kwa viwango vya kitaifa na vile vya kimataifa.

Sambamba na alisema katika mafunzo hayo mawakili hao, watajifunza mbinu za kufungua wa mashauri ya kimkakati na mambo mengine yenye mnasaba na utekelezaji wa haki za binaadamu.

Hivyo, aliwataka washiriki hao kuwa makini  katika mafunzo hayo kwa vile, masuala yaliyopangwa kujadiliwa yanagusa msingi na heshima ya ubinaadamu.

“Haki za Binaadamu ni kati ya vitu vya msingi sana kwa vile yanagusia stahiki ambazo zinampaswa kila binaadamu kuzifaidi kwa kuwa yeye ni binaadamu, haki hizi kwa lugha nyengine huitwa ni haki ambazo binaadamu kuzaliwa nazo,” alisema.

Mapema, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kusimamia kesi zinazohusu masuala ya haki za binaadamu mawakili na kuwasaidia wannachi.

Aidha alisema, mawakili hao watapata uzoefu na kuwasaidia wananchi wanapohitaji kusaidiwa kuendesha mashauri ya haki za kibinadamu na kikatiba.

Alisema, wananchi wanapaswa kutumia njia za busara kudai haki kwa kwenda mahakamani na sio kwenda barabarani kufanya vurugu hivyo wakipata mawakili wa kuwasaidia watadai haki zao mahakamani.